HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 19, 2019

NEC KUANZA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA JULAI

 Na Janeth Jovin

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa Julai mwaka huu inatarajia kuanza zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini kwa awamu ya kwanza kwa kutumia teknolojia ya kieletroniki ya Biometriki. 

Teknolojia hiyo huchukua taarifa za mtu za kibaiolojia na kuzihifadhi katika kanzidata kwa ajili ya utambuzi  na ndio iliyotumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2015.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume Jaji Semistocles Kaijage wakati akifungua mkutano mahususi uliyowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na maofisa wa NEC kwa lengo la kujadili kwa pamoja kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Jaji Kaijage alisema uboreshaji huo wa daftari la kudumu la wapiga kura utawahusu wapiga kura wapya ambao ni watanzania waliofikisha umri wa miaka 18 na  zaidi, wapiga kura walipoteza au kadi zao kuharibika, waliohama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya uchaguzi pamoja na wale wanaorekebisha taarifa zao.

Alisema zoezi hilo la uhakiki wa vituo kwa upande wa Tanzania Bara liliongeza vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 36,549 hadi 37,407 na kwa upande wa Tanzania Zanzibar vituo vimeongezeka kutoka 380 hadi 407.

"Maandalizi mengine yaliyofanyika ni uboreshaji wa majaribio ambao ulilenga kutoa picha halisi ya uwezo wa vipuli vipya vilivyofungwa katika BVR Kits ikiwa ni pamoja na mfumo wa uandikishaji wapiga kura ambao utatumika katika zoezi rasmi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litakaloanza hivi karibuni, " alisema. 

Alisema tume iliendesha zoezi la uboreshaji wa majaribio katika kata ya Kihonda iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kata ya Kibuta iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ili kupata mazingira tofauti ya kijiografia pamoja na idadi ya watu. 

"Uboreshaji huu wa majaribio umefanyika kwa mafanikio ambapo wananchi wengi walijitokeza, kwa upande wa uwezo wa vipuli na mfumo wa uandikishaji kumekuwa na mafanikio makubwa hasa upande wa betri za BVR Kits ambazo zimeonyesha uwezo wa kuhifadhi umeme kwa muda mrefu na hivyo kuweza kukabiliana na changamoto ya nishati ya umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayana miundombinu hiyo, " alisema. 

Alisema pamoja na mafanikio hayo kulikuwepo na changamoto mbalimbali ikiwamo ya wapiga kura kutokuwa na uhakika ama kukumbuka majina yao wanapokwenda kurekebisha taarifa zao hivyo kutumia muda mrefu kituoni kutafuta majina yao.

Aidha alisema kwa mara ya kwanza tume imetoa vibali kwa baadhi ya asasi za kiraia kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari hilo la kudumu la wapiga kura. 

"Pia tume imeandaa mwongozo wa utoaji wa elimu hiyo ya mpiga kura ambao asasi hizo za kiraia zitatakiwa kuufuata wakati wote wa uelimishaji umma kuhusu uboreshaji wa daftari, " alisema. 

Hata hivyo alisema katika kipindi cha kuelekea uboreshaji huo wa daftari, vyama vya siasa vimepatiwa orodha ya vituo vya kupigia kura nchi nzima ili viweze kuweka mawakala katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. 

Alisema tume pia itavishirikisha vyama vya siasa katika eneo la kuteua watendaji wa uboreshaji vituoni ambao ni waandishi wa vituo, wasaidizi wa BVR Kits operators ambapo vyama vitapewa orodha ya majina ya watendaji hao ili vitoe maoni yao.

No comments:

Post a Comment

Pages