HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 19, 2019

NEMC YATOA AGIZO KWA WAMILIKI WA KUMBI ZA STAREHE, BAA NA NYUMBA ZA IBADA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeagiza wamiliki wote wa kumbi za starehe, Baa pamoja na nyumba za Ibada kuhakikisha wanadhibiti uchafuzi wa kelele katika maeneo ambayo ni makazi ya watu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka (pichani), amesema NEMC imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi sehemu mbalimbali nchini kutokana na kushimili kwa kelele na mitetemo chafuzi.
 
"Tumepokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali juu ya kelele na mitetemo chafuzi zinazotoka katika maeneo ya Kumbi za starehe, baa pamoja na nyumba za ibada,"alisema Dkt Gwamaka.
 
Dkt Gwamaka alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake zinakataza uwepo wa kelele na mitetemo chafuzi
Sheria na kanuni hizo zinakataza uwepo wa kelele na mitetemo chafuzi, hivyo ni vyema shughuli hizo zikaendeshwa katika maeneo yaliyorasimishwa au katika majengo yaliyojengwa katika muundo wa kudhibiti sauti zisitoke nje na kuwa kero kwa wananchi wa eneo husika, alisisitiza Dkt Gwamaka.
 
Hata hivyo NEMC imebaini kuwa tatizo hilo limechangiwa na Kumbi hizo, baa pamoja na nyumba za ibada kujengwa kwenye makazi ya watu.
 
Katika utafiti wetu, tumegundua kuwa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na ujenzi holela usiofuata sheria ya mipango miji hali ambayo ni rahisi sana kukuta viwanda, nyumba za kuabudia na kumbi za starehe katika makazi ya watu, alifafanua Dkt Gwamaka.
 
Agizo hilo limeungwa mkono na baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti kuonyesha kukerwa na uchafuzi huo wa kelele katika maeneo ya makazi hususani kwa nyakati za usiku.
 
“Binafsi naunga mkono tamko hili la NEMC kwa kuwa limekuja katika wakati ambao linauhitaji kwa wananchi kwani tumekuwa tukiathirika na uchafuzi wa kelele hususani kwa mikesha ya miziki na ibada zinazofanyika katika maeneo ya wazi ambayo pia ni makazi ya watu, alisema Bwana Yasini Mbalami mkazi wa Mbagala Kuu.
 
Mohammed Twaha ambaye ni mkazi wa Kigamboni kwa upande wake licha ya kupongeza tamko hilo la NEMC, alisema kuwa limechelewa kutolewa kwani maeneo mengi yamekuwa yakiathirika na kelele hizo zinazotokana na ala za muziki kutoka kwenye kumbi za starehe.
 
"Huku mitaani hali ni mbaya, kumbi za starehe na wakati mwingine ni maeneo ya wazi imekuwa ni wazalishaji wakubwa wa uchafuzi wa kelele hali inayotufanya tushindwe kulala vizuri hasa kwa wakati wa usiku", alisema Bw. Twaha.
 
Hata hivo NEMC imefanunua kuwa tamko hilo halihusu ibada fupi kama vile Adhana misikitini, Kengele za kanisani ambazo huita waamini kwenda kufanya ibada pamoja na ibada za muda mfupi.

No comments:

Post a Comment

Pages