HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 17, 2019

WEMA SEPETU ATUPWA GEREZANI SIKU NANE

 Msanii wa Filamu Wema Sepetu akitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo baada ya mahakama hiyo kutoa maamuzi ya kwenda Gereza la Segerea kwa siku nane. Wema aliingia matatani baada ya kutofika mahakamani hapo mara mbili hivyo mahakama ilitoa hati ya kumkamata kwa kuruka dhamana.
 Msanii wa Filamu Wema Sepetu akiingia katika gari la magereza.
Wema Sepetu akipaelekea kupanda gari la magereza baada ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa maamuzi ya kwenda Gereza la Segerea kwa siku nane.
 
Na Janeth Jovin

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru msanii wa filamu Wema Sepetu kukaa gerezani kwa siku nane wakati akisubiri maamuzi ya dhamana.

Wema aliingia matatani baada ya kutofika mahakamani hapo mara mbili hivyo mahakama ilitoa hati ya kumkamata kwa kuruka dhamana.

Akitoa maamuzi hayo leo, Hakimu Mkazi, Maira  Kasonde alisema kutokana na masuala yaliyoletwa mahakamani hapo yanahusu dhamana, atatoa uamuzi.

Alisema kesi hiyo itakuja Juni 24, mwaka huu hivyo mshitakiwa anatakiwa kukaa ndani hadi tarehe hiyo. 

Akijitetea kwanini  asifutiwe dhamana, Wema alidai ni kweli hakufika mahakamani Mei 11 na Juni 14, mwaka huu, ambapo alidai mara ya kwanza alisafiri kikazi nje ya mkoa ambapo alikwenda mkoani Morogoro na kwamba alimpa taarifa wakili wake.

Alidai mara ya pili, alifika mahakamani lakini alishindwa kuingia kwenye chumba cha mahakama kusikiliza kesi yake kwa sababu aliumwa ghafla tumbo la hedhi.

Alidai anapofika tarehe ya hedhi mara nyingi tumbo humuuma hivyo alienda hospitali kwa ajili ya kuchomwa sindano ya diclopa. Hata hivyo, aliomba mahakama imsamehe kwa kutokuhudhuria mahakamani.

Wakili wa Serikali, Glory Mwenda alidai mshitakiwa hana rekodi yakutohudhuria mahakamani hivyo mahakama impe onyo.

Pia alimtaka mshitakiwa endapo atapata udhuru kuwapa taarifa wadhamini wake ili kuepuka usumbufu kwa mahakama.

Juni 11, mwaka hu upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Sylvia Mitanto ulidai kwamba mshitakiwa hayuko mahakamani na hakuna taarifa yoyote.

Wema anakabiliwa na mashtaka ya kusambaza  video ya ngono katika mitandao ya kijamii kupitia simu yake ya kiganjani.

Wema anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, ambapo alisambaza video za ngono kupitia akaunti yake ya Instagram, picha ambazo inadaiwa kuwa haina maudhui.

No comments:

Post a Comment

Pages