HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 14, 2019

BENKI YA CRDB YAPELEKA WATEJA 70 KUJIFUNZA MAONYESHO YA BIASHARA CHINA

BENKI ya CRDB kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) imeandaa ziara ya wateja wake 70 kutembelea maonesho ya biashara ya Canton nchini China.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Meneja Mwandamizi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Rehema Shambwe, amesema ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Benki ya CRDB katika kuwajengea uwezo wateja wake
wajasiriamali jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi katika biashara zao.

“Pamoja na huduma ambazo tumekuwa tukiwapatia ikiwamo mikopo ya uwekezaji na uendeshaji biashara zao, bado tunaona kuna umuhimu kwao kujifunza kwa wenzetu nchi zilizoendelea wanafanyaje ili na wao waweze kuboresha zaidi biashara zao. Ni matarajio yetu watajifunza vitu vingi na sisi tutakuwa nao kuwasaidia kufikia lengo,” alisema Bi. Shambwe.

Pia alizungumzia utayari wa Benki ya CRDB katika kusaidia wajasiriamali nchini Bi. Shambwe alisema mwaka 2005 Benki ya CRDB ilikuwa Benki ya kwanza nchini kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali ambapo mpaka sasa zaidi ya wajasiriamali 30,000 nchini wameweza kunufaika na mikopo kwa ajili ya kuendeleza na kukuza biashara zao.

“Pamoja na dawati la Wajasiriamali tuna madawati maalum kwa ajili ya biashara, tuna dawati la China na India kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara kufanya biashara kwa urahisi zaidi,” aliongezea Bi Shambwe huku akisema kuwa Benki hiyo inatoa fursa za kipekee kwa wakinamama kupitia mikopo ya wakina mama wajasiriamali ijulikanayo kama WAFI. 

Naye Mwenyekiti wa TWCC Jacqueline Maleko ambaye pia ni mmoja wa wateja walionufaika na mpango huo wa Benki ya CRDB aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwathamini na kuwajengea wajasiriamali uwezo, huku akiwataka wafanyabiashara wengine katika ziara hiyo kutumia fursa hiyo kujifunza vitu ambavyo vitakwenda kuboresha biashara zao.

Ziara hii inakuja katika kipindi ambacho Benki ya CRDB imezindua kampeni maalum ijulikanayo kama “Ulipo Tupo” ikielezea ni jinsi gani Benki hiyo imejipanga viliyo kuwahudumia Watanzania katika kila hatua ya maisha yao ili kufikia lengo lakuboresha maisha ya kila Mtanzania.


Meneja Mwandamizi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Rehema Shambwe, akipeana mkono na Kaimu Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kwenda China katika Maonesho ya Biashara ya Canton. Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) imeandaa ziara ya wateja wake 70 kutembelea hayo.

Meneja Mwandamizi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Rehema Shambwe, akibadilishana mawazo na Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Jacqueline Maleko (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi TWCC, Mwajuma Hamza, (katikati).

Kaimu Mkurugenzi TWCC, Mwajuma Hamza (katikati), akibadilishana mawazo na Meneja Mwandamizi wa Wateja Wadogo na wa Wakati wa Benki ya CRDB, Rehema Shambwe (kulia) na Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Jacqueline Maleko (kushoto).

Meneja Uhusiano wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Elizaberth Mgaya (kulia), akisalimiana na wateja wa benki hiyo.

Meneja Uhusiano wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Elizaberth Mgaya (wa pili kulia), akiwa katika picha ya pamoja na wateja wa benki hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kabla ya safari kwenda China kutembelea maonesho ya biashara ya Canton.

Mfanyabiashara Samweli Mchome, akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa safari yao.

Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Jacqueline Maleko, akizungumzia namna Benki ya CRDB ilivyofanikisha safari yao.

Kaimu Mkurugenzi TWCC, Mwajuma Hamz, akizungumza na waandishi wa habari.

Viongozi wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara wanaokwenda kutembelea maonesho ya biashara ya Canton nchini China.

No comments:

Post a Comment

Pages