HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 16, 2019

Ufaransa, MUHAS waanzisha ushirikiano

 Na Irene Mark

CHUO Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) jana Desemba 14, 2019 kimesaini makubaliano ya shirikiano na Chuo Kikuu cha Bordeaux cha nchini Ufaransa.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Balozi wa Ufaransa Frédéric Clavier na Makamu Mkuu wa MUHAS Profesa Andrew Barnabas wakati wa kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa.

Akizungumza baada ya kutiliana saini, Profesa Barnabas alisema ushirikiano huo utahusu afya ya mazingira na afya sehemu ya kazi.

"Ushirikiano wetu utahusu zaidi afya ya mazingira kwa binaadamu kwenye muingiliano wa watu na mimea...tutaangalia hasa katika mimea na matumizi ya dawa za viwandani zinavyoathiri afya za binaadam.

"...Hawa wenzetu wa Bordeuaux wanauzoefu wa muda mrefu pia ni chuo kikubwa, sisi tuna wanafunzi 4,400 kwa mwaka wao wana wanafunzi 66,000 wa fani tofauti kwa wakati mmoja.

"Makubaliano haya yatasaidia sana kwenye tafiti zetu na kukuza kazi za kitafiti lakini pia kusaidia kwenye kutunga sera katika kusaidia taifa kukinga afya za binaadam na maradhi tunayoweza kudhibiti," alisema Profesa Barnabas.

Kuhusu ushirikiano huo, Balozi Clavier alisema ni furaha ya taifa lake kushirikiana na Tanzania huku akisisitiza kwamba ufadhili wa masomo watakaopata watanzania utaleta manufaa taifa hili chimbuko la lugha ya Kiswahili.

Katika makubaliano hayo pia, Ufaransa imefungua milango kwa watanzania zaidi kusoma nchini kwao kwa kuongeza nafasi za ufadhili kutoka 30 kwa mwaka hadi 50.

Imeelezwa kuwa nafasi hizo ni tofauti na zile zinazotolewa na taasisi na mashirika yaliyopo Ufaransa ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano uliodumu kwa miaka mingi.

Kongamano hilo lilishirikisha wanafunzi zaidi ya 900 waliojadiliana masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kupata ajira katika kampuni 40 za uwekezaji zilizopo nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages