November 21, 2020

Uswisi yaridhishwa na miradi ya USMJ vijijini

Wadau wa uhifadhi wa misitu na mazingita wakiwemo Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili
Tanzania(TFCG) Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania(MJUMITA), maofisa wa idara mbalimbali za mazingira kutoka serikalini pamoja na maofisa wa ubalozi wa Uswisi wakiwa katika kikao cha utambulisho baada ya kufika ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa.

Mkuu wa Idara ya Ajira na Kipato kutoka Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania Peter Sidler(kulia)akiwa na maofisa wengine wakijadiliana jambo kabla ya kuingia katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Elia Luvanda akizungumza mbele ya wadau wa uhifadhi wa misitu na mazingira. Aliyekaa ni Mkurugenzi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) Charles Meshack.

 

NA SULEIMAN MSUYA, IRINGA


NCHI ya Uswisi imesema inaridhishwa na mafanikio ya Miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii Tanzania (USMJ) ambayo inatekelezwa nchini.

Miradi ya USMJ inatekelezwa chini ya Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) na Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST) chini ya  ufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) na kuratibiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTEDO).

Akizungumza katika ziara ya wajumbe wa kamati ya ushauri ya mradi iliyotembelea Kijiji cha Mahenge kilichopo Kata ya Mahenge, Tarafa ya Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa, Mkuu wa Idara ya Ajira na Kipato kutoka Ubalozi wa Uswisi, Peter Sidler amesema ameridhishwa na miradi ambayo wanafadhili jambo ambalo linawapa nguvu kuendelea kufadhili.

Sidler amesema ushirikiano wa Tanzania na Uswisi una zaidi ya miaka 30 hivyo matarajio yao ni kuendeleza hasa kwa kugusa kundi kubwa la jamii vijijini.

Mwakilishi huyo amesema takwimu zinaonesha Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa uharibifu wa misitu hivyo miradi ya USMJ inayotekelezwa inapaswa kuungwa mkono ili kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema shughuli za uhifadhi zinazofanyika Kijiji cha Mahenge zimeonesha picha nzuri kuwa jamii ipo tayari kutunza na kuhufadhi misitu yao na kunufaika hivyo wataendelea kuwezesha taasisi kama TFCG na MJUMITA ili kuendeleza malengo ya wanavijiji.

Mkuu huyo wa idara amesema misitu ikitumiwa kwa dhana shirikishi itachochea mabadiliko makubwa ya kiuhifadhi, kiuchumi, kijamii na maendeleo.

"Sisi kama Ubalozi wa Uswisi tunaridhishwa na hali ya USMJ inayotekelezwa kwa vijiji vya mradi jambo ambalo linatupa nguvu kuendelea kufadhili kwani ni njio muhimu ya kupunguza umaskini na kuongeza uhifadhi," amesema.

Sidler amesema wao kama ubalozi wanasaidia sehemu kidogo ya uhifadhi na kuboresha maisha ya wananchi lakini jukumu kubwa lipo chini ya Serikali na wananchi wenyewe.

Amesema ni vema wadau wote wakashiriki katika uhifadhi ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yana madhara makubwa duniani kwa sasa.

Mkuu huyo wa idara amesema mwitikio wa wananchi katika USMJ ni mkubwa hivyo ni jukumu la viongozi kushirikiana nao ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha, amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha sekta zote zinahusika katika kuondoa umaskini.

Amesema Tanzania imejaliwa misitu mingi ambayo ikitunzwa vizuri itaweza kuchochea uwepo wa hali ya hewa nzuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFCG, Charles Meshack amesema Tanzania ina hekta milioni 48.8 za misitu ambapo hekta milioni 22 ipo katika ardhi za vijiji ambapo hekta milioni 5 ndio ipo kwenye USMJ huku hekta milioni 17 zikiwa hazipo kwenye usimamizi.

Amesema TFCG na MJUMITA wameamua kuja na mradi wa TTCS NA CoFoREST ili kuwezesha wananchi kutambua umuhimu wa utunzaji wa misitu.

Meshack amesema iwapo hakutakuwa na jitihada za kuhifadhi misitu ni wazi kuwa ndani ya miaka 40 ijayo misitu itatoweka kwani kwa sasa kila mwaka hekta 469,000 zinapotea.

"Miradi hii ambayo tunawapelekea wananchi ina malengo makuu matatu ambayo ni kuhamasisha wananchi kuhifadhi misitu ya asili na kuvuna kwa uendelevu na wanapovuna kwa undelevu kipato wawekeze kwa shughuli za wananchi na uhifadhi.

Kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili nchi isiwe jangwa. Lengo kubwa ni kuwapa wanavijiji motisha wananchi wasigeuze misitu mashamba badala yake waweze kuvuna kwa uendelevu mkaa na mbao," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema miradi ya USMJ ambayo wameibua kwa taktibani miaka saba sasa imeweza kuchochea maendeleo, kukuza uchumi na kuchochea uhifadhi.

Meshack amesema katika vijiji zaidi ya 30 ambvyo vinatekeleza mradi vimeweza kuboresha sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na mikopo ambapo wanavijiji wamekusanya zaidi shilingi bilioni 3.

"Tumewekeza takribani bilioni 12 kwa awamu ya kwanza na pili lakini pia zaidi ya sh.bilioni 3 zimepatikana," amesema.

Amesema awamu hii ya tatu wanatarajia kuwekeza shilingi bilioni 7 kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo wanajikita kujengea uwezo wataalam ili ziweze kutekeleza zenyewe.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia miradi hiyo wamefanikiwa kurasimisha ardhi za vijiji kuwa za kisheria jambo ambalo linatoa uhakika wa kupangia kazi kisheria.

Amesema Serikali inapaswa kutoa kipambele katika sekta ya mazingira na misitu ili iweze kuwa endelevu na kuondoa sheria vikwazo katika kusimamia misitu akitolea mfano GN417.

Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahima Njaidi amesema TFCG na MJUMITA zimedhamiria kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya misitu na mazingira nchini

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda amepongeza nchi ya Uswisi, TFCG, MJUMITA na wadau wengine wanapigania USMJ kwani ni muhimu kwa maendeleo nchini.

Luvanda amesema Mkoa wa Iringa utashirikiana na wadau wote ambao wamedhamiria kuhifadhi na kutunza misitu kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo, uchumi, kisiasa na kijamii.

Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa amewataka wanakijiji wa Mahenge kutumia fursa ya mradi huo kufanya mabadiliko chanya kijijini hapo.

"Mimi nipo Morogoro natambua faida za hii miradi nawaomba msirudi nyuma kwani ina faida ya kiuchumi, kijamii, maendeleo na uhifadhi," amesema.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFORI), Dk.Charlestino Balama amewashauri wataalam na wananchi kutafuta watafiti ili kuweza kubaini fursa zote zilizopo katika misitu wa Mahenge.

"Watafiti tunapaswa kuja huku kwenye Msitu wa Mahenge kwani kuna fursa nyingi nimeziona hapa kama kuwepo vipepeo, ufugaji nyuki, madini na vingine vingi," amesema.

Akizungumzia mradi huo Mtaribu wa Mradi  wa CoFoREST Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Aigen Mwilafi amesema mradi huo umewezesha uandaaji wa mipango ya USMJ na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Aidha ametoa ombi kwa TFCG pamoja na wadau wake waendelee kuiwezesha halmashauri hiyo katika suala la uhifadhi wa misitu ya vijiji kwa kuitenga na kuhuwisha mipango ya usimamizi shirikishi ya vijiji iliyopitwana wakati.

Aidha amesema kuna takribani misitu 11 haijatengwa kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji na kuna mipango ya usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji 45 imepitwa na wakati inahitaji kuhuhishwa.

Hivyo wangependa misitu yote katika vijiji vyao itengwe na kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji na iwe na mipango iliyohuwishwa na kupitishwa katika ngazi zote za kisheria.

"Tunaomba muendelee kushirkiana nasi katika kutekeleza hayo," amesema.

Ametumia nafasi hiyo kueleza TFCG imekuwa ikifanya kazi za uhifadhi kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Kololo tangu mwaka 2007 na kwamba TFCG na MJUMITA kwa kushirikiana na halmashauri iliunda mtandao mitandao ya jamii ya usimamizi wa misitu ya asili minne.

Ameongeza na kuanzisha mpango wa uvunaji wa mazao wa mazao ya misitu wa Wilaya.Pia kuanzisha mitandao mingine mipya katika kata za Mahenge na Nyanzwa na kwamba mwanzoni mwa Machi 2020 timu ya watalaam wa mradi kwa kushirikiana na halmashauri walitembelea vijiji vya Ikula, Mahenge, Mgowelo na Udekwa kwa lengo la kutembelea misitu na kuona kama inakidhi vigezo vya kutekelezwa mradi wa mkaa endelevu na kuzungumza na viongozi wa vijiji husika.

"TFCG na wadau wake kupitia mradi huu ,mpaka sasa imeweza kuwajengea uwezo watalaam 17 kutoka ngazi ya halmashauri  na wanne kutoka ngazi ya kata kwa kutoa mafunzo mbalimbali. Kijiji cha Mahenge ambacho ndicho kinatekeleza mradi huu kumefanyika mikutano ya vitongoji kwa ajili ya kuutambulisha mradi.

"Pia kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi, mipango ya usimamizi shirikishi wa misitu ya kijiji na kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.Kuna mafunzo yanaendelea ya uzalishaji mkaa endelevu na uzalishaji wa mbao,kwa wazalishaji mkaa na wapasuaji mbao ambao walikuwa wanajishughulisha na shughuli hizo hapa kijijini bila kufuata taratibu,"amesema Mwalifi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo Said Mhina amesema wameomba msaada wa kupatiwa mafunzo zaidi ambapo amefafanua licha ya kuelimishwa bado wanaomba waendelee kupatiwa elimu zaidi na kwamba wanamini kile ambacho kitapatikana kitasaidia kuleta maendeleo ya kijiji chao.

No comments:

Post a Comment

Pages