NA, TIGANYA VINCENT, TABORA
SERIKALI imetoa jumla ya shilingi bilioni 8.8 kwa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kukarabati na
kujenga Hospitali na Vituo vya Afya katika kipindi cha 2015 hadi Desemba 2019
ili kusogeza huduma za utoaji wa tiba kwa wananchi.
Hatua hiyo imeondoa adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu
kutafuta huduma za afya na kurahisi upatikanaji wa vifaa tiba na huduma za
upasuaji katika maeneo yaliyo karibu na wanapoishi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Wajumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa
wa Tabora.
Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 3 zimetumika
kujenga Hospitali za Wilaya ya Sikonge na Uyui
ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 97.
Mwanri alisema kuwa shilingi bilioni 1 zilitumika katika
kukarabati Vituo vya Afya vya Zogolo cha Halmashauri ya Nzega Mji, na Upuge cha
wilaya ya Uyui.
Alisema kuwa shilingi bilioni 4.8 zimetumika katika ujenzi na
ukarabari wa Vituo vya Afya vya Simbo cha Igunga, Ulyankulu cha Kaliua , Ussoke
cha Urambo, Kitunda na Kipili vya Sikonge, Busondo cha Nzega na Ussoke Mlimani
cha Urambo.
Mwanri aliongeza kuwa vituo vingine ni Igurubi cha Igunga,
Maili Tano kilichopo Manispaa ya Tabora, Igalula cha Wilayani Uyui na ujenzi wa
Wodi ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega.
Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya
Urambo Obed Balola alizitaka Halmashauri ya Wilaya ya mbalimbali kuongeza
juhudi kuandika wananchi wanaojiunga na Mfuko Afya ya Jamii(CHF) ili waweze
kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Alisema Mkoa wa Tabora una ya Kaya 421,023 ambapo hadi hivi
sasa kuna kaya 5,780 ambapo ni wananchi 29,713 ndio wananufaika na huduma hiyo.
Balola alisema idadi hiyo ni kidogo jambo ambalo linaonyesha
kuwa watu wengi bado hawana uhakika na huduma za afya.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali
ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
miradi mbalimbali ikiwemo ya afya.
No comments:
Post a Comment