HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 20, 2020

CCM TABORA YAAGIZA HALMASHAURI KILA MWEZI KUTENGA ASILIMIA 10 KWA AJILI YA MIKOPO

NA TIGANYA VINCENT
 
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora kimezitaka Halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha zinatenga kila mwezi asilimia 10 ya fedha zinazotokana na mapato yake ya ndani kwa ajili ya utoaji wa mikopo. 
 
Azimio hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tabora wakati wakipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
 
Alisema ni lazima kila wapokusanya watenge asilimia 10 za kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu kama wanavyotakiwa badala ya kusubiri hadi ipite miezi mingi ndipo watoe mikopo.
 
Wakasuvi aliwashauri kuwa wakati utoaji wa mikopo ni vema wakawashirikisha Viongozi wa CCM katika maeneo yao ili wakati wa kudai wawasaidie na pia watoe elimu juu ya umuhimu wa kurejesha fedha hizo.
Aidha Mwenyekiti huyo alisema kuwa kuanzia sasa watakapokuwa na ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa watakagua miradi inayotokana na asilimia 40 za makusanyo ya ndani.
 
Alisema kuwa lengo ni kutaka kujiridhisha kama kweli Halmashauri zinatenga asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili wawe kujua  mchango wa fedha za Serikali kuu na ule wa  Halmashauri katika mradi lengwa.
 
Wakasuvi alisema upo uwezekano wa Halmashauri kutofanya chochote kwa kipindi cha miaka mitano kupitia fedha zake za ndani.
 
“Kuna ziara zijazo tumekusudia kutembelea miradi inayotokana na asilimia 40 ya makusanyo ya ndani ili tuweze kuona thamani halisi ya fedha zilizotumika na kama kweli fedha zinatengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo…hata kama Serikali Kuu imechangia fedha ni vema waeleze ni kiasi gani ? na wao wamechangia kiasi gani? “ alisisitiza.
 
Alisema kwa upande wa miradi iliyotokana na fedha za Serikali kuu wameridhika na matumizi yake na ndio maana sasa wanataka kujielekeza katika kukagua miradi inayotokana na fedha za ndani za Halmashauri.

No comments:

Post a Comment

Pages