HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 20, 2020

Wakazi 130 wasubiria fidia kwa miaka mitano

Mkazi wa Mtaa wa Mikongeni, Mji mdogo wa Kibaha, mkoani Pwani, Fines Lema, akionyesha nguzo inayoshikilia nyumba yake isianguke kutokana na kutotakiwa kuyaendeleza maeneo hayo. (Na Mpiga Picha Wetu).
 
 
Na Mwandishi Wetu
 
WAKAZI zaidi ya 130 wa Kata ya Viziwaziwa Mji mdogo wa Kibaha mkoani Pwani wapo hatarini kupoteza maisha kutokana na kuishi katika mazingira hatarishi baada ya serikali kuchukua maeneo yao kwa ajili ya mradi mpya wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400.
Wakizungumza na TanzaniaDaima juzi baadhi ya wakazi hao, walisema kuwa huu ni mwaka wa tano tangu serikali iwafanyie tathimini ya maeneo yao kwa ajili ya mradi huo unaotoka jijini Dar es Salaam mpaka Arusha kupitia mikoa ya Pwani, Tanga na Kilimanjaro, mradi unaofadhiliwa na benki ya Exim ya China.
Wananchi hao walisema, kuwa serikali imewafanyia tathimini mara tatu tangu mwaka 2016 kwa ajili ya kuwalipa fidia lakini hadi sasa kuna sintofahamu kuhusiana na suala hilo.
Mkazi wa Mtaa huo, Venance Kanoga ambaye anasumbuliwa na tatizo la moyo, akizungumza kwa shida alisema, mazingira wanayoishi kwa sasa ni mbaya kwa kuwa serikali imewarudisha nyuma kimaendeleo kutokana na kuchukua maeneo hayo bila kuwalipa hadi sasa.
“Hapa unaponiona ninatatizo la moyo, natakiwa kutibiwa, sina fedha na mali nilizokuwa nikizitegemea zote zimeteketea, serikali imechukua maeneo yetu na hatutakiwa kuyaendeleza wala kuyauza, alisema na kuongeza kuwa
…Iwapo maeneo yangu yasingechukuliwa na serikali ningeweza kuuza nikapata fedha ya kujitibu na hata kuwa na biashara ya kufanya lakini kwa sasa nashindwa nimebaki maskini.”
Naye Mkazi wa mtaa huo, Abbilloye Freka alisema, kuwa suala hilo wamejaribu kulifuatilia kila mahali bila kupata majibu ya kuridhisha hivyo wanaiomba serikali iwapatie fidia hiyo ili waweze kuendesha maisha yao.
“Suala hilo tumefuatilia kila mahali tulianza kwa kuunda Kamati ya watu watano iliyokwenda kwa Mkuu wa Mkoa, tukaelekezwa kwenda kwa uongozi wa Tanesco tukakutana na Injinia wa miradi ya uwekezaji Tanzania ambaye alitupa barua na kusema suala letu lipo Wizara ya Fedha na Mipango,” alisema.
Freka alisema kuwa, Tanesco iliweka wazi kuwa suala hilo halipo mikononi mwao hivyo wanaopaswa kulijibia ni Hazina ambao wanapaswa kuwalipa fedha za kupisha mradi huo.
Naye Fihanes Lema mkazi wa mtaa huo anasema kuwa serikali inapaswa kuwalipa fedha hizo ili waondokane na kukaa maporini na kuishi katika makazi hatarishi.
“Kwa kweli hali yetu ni mabaya, makazi tunayoishi ni hatari sana mvua zikinyesha hatuna amani maana tunahofu ya kuangukiwa na ukuta, tunaiomba serikali itulipe ili nasi tuweze kujikwamua,” alisema.
George Makene mkazi wa mtaa huo alisema kuwa, viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa kauli kuhusiana na malipo hayo kuwa tayari lakini cha ajabu sasa inakwenda mwaka wa tano lakini hakuna malipo.
Makene alisema kuwa, pamoja na kufanyiwa tathimini lakini serikali hadi sasa haijaweka wazi kiasi cha malipo kitakacholipwa kwa wakazi hao jambo ambalo linawatia hofu ya kuwepo kwa dhuluma ya fidia.
“Tumefanyiwa tathimini mara zaidi ya mbili na mwishoni mwa mwaka jana walikuja ofisa Tanesco na Ofisa Maendeleo ya Jamii katika maeneo haya na kuchukua ‘sample’ ya udongo lakini kuhusu malipo yetu hakuna aliyezungumza na mazingira tunayoishi wanayaona, hii inatusikitisha,” alisema.
Naye Paul Andrew mkazi wa mtaa huo ambaye alisema ameishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30 sasa lakini tabu anayoipata na familia yake ni mbaya zaidi kutokana na serikali kutowalipa fidia ya maeneo yao.
“Hapa nilipo mke wangu kanikimbia kwa kuwa hawezi kuishi chumba kimoja na watoto wakubwa, kwa kweli ucheleweshaji wa malipo hayo yanatusababisha tupoteze heshima kwenye ndoa, naiomba serikali itulipe fidia ili turudishe heshima,” alisema.
Mkazi mwingine Alexander Mushi alisema, kuwa wakazi wa maeneo hayo wanaishi katika mazingira hatarishi kwani mvua zikinyesha nyumba zimekuwa zikianguka kutokana na kukatazwa kufanya maboresho.
“Wengi wakazi wa maeneo haya nyumba wanazoishi ni za hatari na pia vichaka vimeongezeka hivyo wakati mwingine wanyama wa hatari wamekuwa wakiwavamia jambo linalohatarisha usalama wao,”  alisema.
Akizungumzia suala hilo, Diwani wa Kata ya Viziwaziwa, Mohamed Chamba, alikiri wananchi hao kuishi mazingira hatarishi na kuiomba serikali iangalie namna ya kuwalipa fidia wananchi hao.
“Suala hili ninalifahamu na kila ofisi za serikali linajulikana lakini hadi sasa tunavyoongea ni zaidi ya miaka mitano wakazi hawa wanaishi mazingira hatarishi na wamerudi nyuma kimaendeleo hivyo serikali iangalie namna ya kuwalipa ili waweze kufanya maendeleo yao,” alisema.
Alitaja maeneo yaliyopitiwa na mradi huo Mwanalugali, Bokotemboni, Sofu, Mikongeni, Bungo, Viziwaziwa, Sagale, Zogowale, Saeni na Zegereni

No comments:

Post a Comment

Pages