April 21, 2020

Kampuni ya FMJ Hardware Limited yawapatia waandishi ‘Sanitaiza’

Meneja Mauzo wa Kampuni ya FMJ Hardware Limited, Fredrick Sanga akimkabidhi Mwandishi  Mwandamizi wa Gazeti la Mwananchi, Kelvin Matandiko vitakasa mikono kwa niaba ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam. (Picha na Suleiman Msuya).


 Suleiman Msuya
 
KAMPUNI ya  FMJ Hardware Limited ya Buguruni Sheli, Ilala jijini Dar es Salaam imetoa vitakasa mikono (Sanitizer) dazeni 10 kwa vyombo vya habari 10 ili viweze kutumia katika mapambano dhidi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Akikabidhi msada huyo Meneja Mauzo wa FMJ Hardware Limited, Fredrick Sanga alisema wameamua kutoa msaada huo kwa vyombo vya habari ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano hayo.
Sanga alisema kampuni yao inajihusisha na uuzaji wa vifaa  vya ujenzi ndani nan je ya nchi hivyo wameamua kusaidia kundi hilo ambalo linafanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii hivyo vitakasa mikono walivyotoa vitasaidia kwa kiwango fulani.
“Leo Aprili 21 mwaka 2020 tumekutana nanyi ndugu zetu waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa msaada wetu kwenu kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya  ugonjwa wa COVID-19.
Ukweli kampuni yetu inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma wa Watanzania katika masuala mbalimbali yanayotokea nchini.Hata hivyo kwenye hili janga la corona ambalo limesababisha hofu kubwa kutokana na kusababisha maafa makubwa, tumeona ni jukumu letu kuhakikisha kundi hili la waandishi nalo linakuwa salama kwa kujikinga na maambukizi,” alisema.
“Hivyo kwa siku ya leo tumeona haja ya kutoa vitakasa mikono ( Sanitizer) kwa vyombo vya habari kwa ajili ya kuliwezesha kundi Hilo angalau kuwa salama.Tunatambua waandishi wako kazini wakati wote na katika kutekeleza majukumu yao wanakutana na watu mbalimbali, hivyo ni matumaini yetu kuwa Sanitizer hizi zitakuwa sehemu ya kukabiliana na corona kwa waandishi wa habari.
Pia tunaomba kueleza kuwa kampuni yetu tunaendelea kuungana na Serikali ya Awamu ya Tano katika jitihada za kupambana  na ugonjwa huo hatari ambao sio tu umesababisha maelfu ya watu duniani kupoteza maisha lakini pia umechangia kukwamisha shughuli za uchumi.
Ni matumaini yetu wadau mbalimbali nchini wakajitokeza kwa pamoja na kuiunga mkono Serikali kwa kutoa misada ambayo inaweza kusaidia katika kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huu,” alisisitiza.
Aidha, Sanga alitoa ujumbe kwa kada ya uuzaji wa vifaa vya ujenzi pamoja na mafundi ujenzi wote kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto.
Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari Mhariri wa Gazeti la Mtanzania, Bakari Kimwanga aliishukuru FMJ Hardware Limited kuwasaidia vitakasa mikono na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia kundi hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages