Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, akitoa nasaha kwa waandishi
wa Habari (hawapo pichani) wakati wa semina fupi ya waandishi hao
iliyolenga kuwapa elimu juu ya masuala ya kitaalalmu katika kuripoti
habari.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria Semina fupi iliyolenga
kuwapa elimu juu ya masuala ya kitaalamu katika kuripoti habari.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Rukwa Izrael
Mwaisaka (kushoto), akipokea bahasha zilizowekwa barakoa kwaajili ya
Waandishi waliohudhuria semina ya Waandishi wa Habari katika Ofisi ya
mkuu wa mkoa kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa Bernard Malaki (kulia)
ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa huo kutoa vifaa vya
kujikinga kwa Waandishi.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) katika
picha ya pamoja na baadhi ya Waandishi wa habari Mkoa wa Rukwa pamoja na
wataalamu wa afya ngazi ya mkoa.
Rukwa, Tanzania
Mkuu wa
mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amewataka wanahabari mkoani humo kuhakikisha
wanajikinga kwa namna yoyote ile ikiwemo kufuata maelekezo ya wataalamu kwa
kuvaa barakoa pamoja na kunawa mikono yao kwa maji tiririka na sabuni kwani
kazi zao zinahusisha kukutana na watu katika kutafuta habari mbalimbali
zinazohusiana na Corona na habari nyinginezo katika kijamii.
Amesema
kuwa mara kadhaa amekuwa akiwashuhudia wakitumia kipaza sauti kimoja wakati wa
kuwahoji watu na hutumia kipaza sauti hicho kuripoti habari kwenye vyombo vyao,
hivyo amewataka kuwa makini zaidi na kuongeza kuwa kutokana na uwezo mdogo wa
waandishi hao kujikimu kuwa na vifaa vya kujikinga, ametoa wito kwa mashirika
ya serikali na yasiyo ya kiserikali kuona umuhimu wa kuwawezesha wanahabari ili
wafanye kazi zao kwa usalama.
“Muwe makini
sana, vinginevyo maambukizi yatawapata sana, kwasababu ugonjwa huu hauchagui,
hauna Mwanahabari, hauna Mkuu wa Mkoa, hauna DC (Mkuu wa Wilaya), hauna Waziri, hauna
mtu yeyote yule, isipokuwa unapenya kwa mtu ambaye hajachukua tahadhari, na
tahadhari mojawapo ni kuvaa barakoa, Wanahabari vaeni Barakoa kila mahali,
mjilinde, nafahamu wanahabari wa Rukwa uwezo ni mdogo hivyo nitoe wito kwa
amashirika ya ndani na nje ya nchi, tutaanzia na ofisi yangu hapa ya mkoa, Katibu
Tawala utafute hata boksi mbili, tatu tuwape wanahabari ili wajilinde,”Alisema.
Aidha, Wangabo amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha kuwa Taasisi zote ndani ya
Mkoa zinakuwa na Vipima joto (Thermal Scanner) na kuongeza kuwa Mkoa umesambaza
vifaa vya kujikinga (Personal Protective Equipment – PPE) 139 katika
halmashauri nne za mkoa pamoja na kusambaza vipeperushi 12,200 vya kutolea
elimu kwa jamii juu ya ugonjwa wa Corona.
Wangabo
ameyasema hayo katika semina fupi iliyowakutanisha waandishi wa Habari katika
Mkoa wa Rukwa na wataalamu wa afya ngazi ya mkoa pamoja na wadau wa mradi wa
Lishe Endelevu unaosimamiwa na Shirika la Save the Children ambapo katika semina
hiyo waandishi walipata kuelewa aina tofauti za barakoa na utendaji kazi wake,
Elimu ya Lishe ya mtoto katika kipindi hiki ambacho ugonjwa wa Corona umekuwa
tishio pamoja na njia za kufuata wanapotafuta habari kuanzia ngazi ya
halmashauri, Wilaya na mkoa.
Kwa upande
wake Kaimu Afisa Lishe wa mkoa, Teddy Swallo, alitoa ufafanuzi juu ya namna ya
kuendeleza lishe yam toto kutoka kwa mama endapo mmoja kati yao atakuwa
ameambukizwa ugonjwa wa Corona na kusisitiza kuwa mtoto hatakiwi kuachishwa
kunyonya kwasababu ya maambukizi na kusisitiza kuwa mama na walezi wa mtoto
wanawe kabla na baada ya kumshika mtoto na wavae barakoa wakati wa kumhudumia
mtoto.
“Kuna maswali
yanayoulizwa mara kwa mara kuhusiana na unyonyeshaji na ugonjwa Covid – 19,
swali, virusi vya Corona vinapatikana kwenye maziwa ya mama? jibu ni kwamba hadi
sasa tafiti zinaonyesha kuwa virusi vya corona havipatikani kwenye maziwa ya
mama, swali, mtoto aliyepata Covid-19 ataendelea kunyonyeshwa? Jibu ni ndio
ataendelea kunyonyeshwa ili aweze kupata king ana virutubishi muhimu kutoka
kwenye maziwa ya mama yake na muhimu mtoto anayeumwa anyonye mara nyingi zaidi
ya kawaida,” Alisisitiza.
Halikadahalika,
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Emanuel Mtika wakati akijibu swali kuhusu dawa
inayosemekana inatibu Corona ya kuchanganya malimao na tangawizi alisema kuwa,
mchanganyiko huo utamsaidia mtumiaji kusafisha na kuimarisha kinywa chake
lakini sio kujitibu ugonjwa wa Corona na kusisitiza wale wanaojisikia dalili za
mafua makali waharakishe kufika katika vituo vya kutolea huduma na sio kubaki
nyumbani wakitegemea ugonjwa huo utapona wenyewe.
Katika
kuhakikisha elimu ya ugonjwa wa Corona inawafikia wananchi Wangabo
ameshafanya vikao na viongozi wa makundi mbalimbali ya jamii, kuwaelimisha na
kutoa maelekezo kwa viongozi wa kata za mwamabo wa Ziwa Tanganyika zenye
bandari bubu 57, na kuunda timu za wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali 11
kuanzia ngazi ya mkoa hadi halmashauri pamoja na kusimamia uandaaji wa mpango
wa dharura wa kukabiliana na Corona uitwao Regional Covid -19 Contingency Plan
ulioanza utekelezaji wake mwezi Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment