HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 23, 2021

Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila yapokea msaada wa milioni 41


Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru (wa pili kushoto), akipokea msaada wa mashine ya upasuaji macho kutoka kwa Mkurugenzi  wa Taasisi ya Vision Care, Jihye Kim.


NA ASHA MWAKYONDE

TAASISI ya Vision Care inayojihusisha na mapambano dhidi ya matatizo ya upofu wa macho duniani imetoa msaada wa mashine ya upasuaji wa macho (Operating Microscope),katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili-Mloganzila yenye thamani ya milioni 41.

Lengo la msaada huo ni kusaidia hospitali kuendelea kutoa huduma bora za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wa macho wanaofika kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Akipokea msaada huo jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema msaada huo umefika muda sahihi kwani wanauhitaji wa mashine hiyo.

Mkurugenzi huyo amesema mashine hiyo itasaidia kuongeza tija katika huduma hasa Idara ya Magonjwa ya Macho na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendeleza mahusiano baina yao.

"Mbali na mahusiano mema taasisi hii imekuwa ikituunga mkono juhudi za hospitali katika kuboresha huduma za afya kwa kutoa mashine ambayo itasaidia utoaji wa huduma bora katika Idara ya Magojwa ya Macho," amesema Prof. Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila, Catherine Makunja amesema mashine ya upasuaji wa macho ni muhimu kwa kuwa  kila mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji wa jicho lazima mashine hiyo itumike.

“Jicho ni kiungo kidogo ambacho upasuaji wake unahitaji umakini wa hali ya juu na Operating Microscope ndio mashine pekee ambayo itamsaidia daktari kufanya upasuaji”amesema Dk.Makunja

Kwa mujibu wa Dk. Makunja tatizo la macho limeongezeka kwa sasa kutokana na madiliko ya mfumo wa maisha ambapo katika Kliniki ya Magonjwa ya Macho Mloganzila wagonjwa 350 hadi 400 huonwa kwa mwezi na baadhi yao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care, Jihye Kim amesema wanayofuraha kukabidhi msaada huu ambao utasaidia wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi na kuahidi kuendeleza mahusiano ili kuendelea kuboresha huduma.

Februari mwaka huu Taasisi ya Vision Care pia ilikabidhi msaada wa mashine ya uchunguzi wa macho (Slit Lamp Biomicroscope ) yenye thamani ya takribani TZS. 20Mil.

No comments:

Post a Comment

Pages