HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 25, 2021

Kimbunga Jobo

 


NA MWANDISHI WETU 

KITOVU cha kimbunga Jobo kipo umbali wa kilomita 76 mashariki mwa Kisiwa cha Mafia, mwenendo wa kimbunga hicho kilichopo bahari ya Hindi umeonesha. 

Kimbunga hicho sasa kinasafiri kwa kasi ya kilometa 20 kwa saa baharini ambayo ni kasi kubwa kwa mwenendo wa vimbunga. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imedokeza katika taarifa yake kwa Umma kuhusu mwenendo wa kimbunga hicho kwa mchana wa leo.

"Taarifa hii inahuisha taarifa ya kimbunga “Jobo” iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania leo asubuhi Aprili 24, mwaka huu," imesisitiza.

Imesema kutokana na kasi hiyo kubwa, kisiwa cha Mafia na maeneo jirani yanatarajiwa kuanza kupata mvua kubwa mapema zaidi leo jioni .

"Kwa upande mwingine, kuanzia usiku wa kuamkia Jumapili Aprili 25, mwaka huu, maeneo ya kusini mwa mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam yanatarajiwa kupata mvua kubwa wakati maeneo mengine ya Lindi, Mtwara na kisiwa cha Unguja pia yanatarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa siku ya kesho kwa baadhi ya maeneo. 

"Aidha, pamoja na upepo wa kimbunga kupungua kwa kiasi kikubwa, vipindi vya upepo mkali vinaweza kujitokeza hususan wakati wa mvua kubwa," imesisitiza.

TMA imeweka msisitizo kwamba wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza. Izingatiwe kuwa vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko.

No comments:

Post a Comment

Pages