Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Francis Michael akipata maelezo kuhusu elimu ya watu wazima kutoka kwa Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Karibu Tanzania (KTO), Symphrose Makungu wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Elimu ya Watu Wazima linalofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Francis Michael akiwa pamoja na washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Wadau wa Elimu ya Watu Wazima unayofanyika katika Ukumbi wa Nkuruma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Na Mwandishi Wetu
WADAU wa elimu ya watu wazima kutoka nchi za Tanzania, Ethiopia, Uganda, Serbia na Ujerumani wamekutana katika kongamano la kimataifa la kujadili namna bora ambayo itawezesha taaluma hiyo kufanywa kitaaluma.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Francis Michael wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Wanataaluma wa Elimu ya Watu Wazima unaofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katibu Mkuu alisema mkutano huo ambao umejikita katika kujadili nafasi na changamoto za elimu ya watu wazima utawapa nafasi wataalam wa eneo hilo kutoa na maazimio ambayo yatawezesha kuifanya elimu hiyo kuwa ya kisasa na yenye tija.
Dk Michael alisema elimu ya watu wazima imekuwa na mchango mkubwa katika kuondoa jamii katika ujinga, hivyo wizara ya elimu, sayansi na tenkolojia itahakikisha inashirikiana na wadau wote kuhakikisha inakuwa endelevu.
“Leo hii wadau wa elimu ya watu wazima wamekutana hapa Nkrumaha UDSM kujadili namna ya kufanya taaluma hii iwe ya kitaaluma zaidi, ili lengo lankutoa ujinga kwa Watanzania,” alisema.
Katibu huyo alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 20 ya Watanzania bado wapo kwenye dimbwi la kutokujua kusoma na kuandika, hivyo kupitia mkuatano huo wa kimataifa wadau wataweza kutoka na maazimio sahihi ya kufikia asilimia 100.
Dk Michael alitoa rai kwa wananchi ambao hawakufanikiwa kupata elimu wajitokeze kupata elimu na maarifa ambayo yanatolewa kwenye vyuo vya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la DVV la nchini Ujerumani.
Alisema kinachofanywa na DVV ni katika kuendeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuruhusu wanafunzi ambao waliacha kusoma kurudi kusoma.
Kwa upande wake, Profesa Eustella Balamsesa wa Shule Kuu ya Elimu UDSM alisema kongamano hilo linatarajiwa kutoa mwanga wa kuendeleza elimu ya watu wazima hapa nchini.
Alisema kongamano hilo pamoja na kuwapa nafasi wadau kujadili namna ya kuendeleza elimu ya watu wazima, pia wanatumia nafasi hiyo kutambulisha makao makuu ya DVV ambayo kwa sasa yatakuwa hapa nchini.
“Mwezi Juni 2022 kulikuwa na mkutano wa kimataifa jijini Marrakech Morocco pamoja na mambo mengine, wanachama wa elimu ya watu wazima walikubaliana kila nchini inahakikisha kunakuwa na wataalam wa taaluma hiyo,” alisema.
Profesa Balamsesa alisema mikakati ya elimu ya watu wazima kwa sasa sio kusoma na kuandika, bali ni kuhakikiasha wahusika wanapata elimu yenye ujuzi, maarifa na mbinu za kuchangia maendeleo endelevu.
Alisema elimu ya watu wazima katika miaka ya zamani ilikuwa na tija, ila kwa siku za karibuni imekuwa tofauti, hivyo wanatarajia kupitia DVV wanaenda kurejesha dhana nzima ya elimu hiyo.
Mkurugenzi wa Ofisi ya DVV nchini Ujerumani alisema wanafanya kazi katika nchi 30 ikiwemo Tanzania, lengo likiwa ni kusadia wananchi wenye uhitaji wa elimu ya watu wazima wanatekeleza dhamira yao.
Alisema wamelazimika kuweka makao makuu ya DVV nchini Tanzania ili kushirikiana na Serikali kuwafikia wahitaji wote wa elimu ya watu wazima.
Naye Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Karibu Tanzania (KTO), Symphrose Makungu alisema kongamano hilo limefanyika wakati muafaka na kwamba watashiriki kikamilifu kuhakikisha malengo ya elimu ya watu wazima yanatimia.
“KTO inashirikiana na
DVV kutoa elimu ya watu wazima kupitia vyuo vya maendeleo ya jamii nchini na
mwitikio ni mzuri ni imani yetu asilimia 20 ya wasijua kusoma na kuandika
itapatiwa ufumbuzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment