.......................................................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKURUGENZI
Mkuu wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James Mataragio amewataka watanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na ujenzi wa
bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania ili
kujiongezea kipato na utaalam kwani sehemu kubwa ya bomba hilo linapita nchini
Tanzania.
Mataragio
ameyasema hayo leo Septemba 14, 2022 wakati
akikagua maandalizi ya ujenzi wa mradi huo uliopo eneo la Ntondo mkoani Singida
ambao upo katika hatua ya kuandaa eneo zitakapo jengwa nyumba watakazokuwa
wakikaa watu zaidi ya 500 watakaokuwa wakifanya kazi katika mradi huo.
Alisema
eneo hilo yatakuwa yakihifadhiwa mabomba ambayo yatachomelewa Sojo na yakifika
hapo yatakuwa yakisambazwa kwenye mkuza kutokea mkoani Kagera hadi Tanga na
katika makambi mengine 14.
“
Mradi huu ni wa muhimu kwa nchi yetu kwani asilimia, 80 ya bomba hili
lipo upande wa Tanzania hivyo nawaomba watanzania wachangamkie fursa zitakazotokana
na utekelezaji wa mradi huu” alisema Mataragio.
Alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo mkoani hapa inakadiriwa zaidi ya ajira 500 zitapatikani ambapo aliomba wahusika wa mradi huo kutoa upendeleo wa ajira hizo kwa wananchi wa mkoa wa Singida hasa wale wanaoishi jirani na eneo la mradi.
Alisema Serikali ilisaini Mkataba wa Msingi wa Mradi (Host Government Agreement (HGA) kati yake na Mwekezaji, Kampuni ya EACOP ambapo, kupitia Mkataba huo umeainisha baadhi ya huduma na bidhaa zitakazotolewa na Watanzania pekee ikiwemo huduma za usafirishaji, ulinzi, chakula na vinywaji, huduma za malazi na usambazaji wa mafuta kwa ajili ya magari na mitambo.
Amezitaja
huduma nyingine kuwa ni pamoja na shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana hapa
nchini, shughuli za ujenzi, huduma za mawasiliano na ukodishaji wa mitambo ya
ujenzi.
Dk.
Mataragio alisema kazi za fidia zimeanza kufanyika kwa maeneo yote
yanayopitiwa na bomba katika sehemu zinapofanyika kazi maalum na kuwa maeneo
mengine kma kule Sojo tayari wameshalipwa fidia zao na kujengewa nyumba zao baada
ya kuhamishwa kupisha mradi.
Dk. Mataragio aliwataka
wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa
na si vinginevyo kwani uzoefu unaonesha baadhi yao wamekuwa wakishindwa hadi
kufikia serikali kuwanyang’anya miradi.
Katika hatua nyingine Dk. Mataragio alikwenda kumtembelea mnufaika wa mradi huo Mzee Juma Hamisi Mwengo ambaye alikubali
kutoa eneo lake kwa ajili ya kupisha mradi huo ambapo Serikali imemjengea nyumba ya
kisasa.
Mzee Mwengo alitoashukurani zake kwa Serikalikwa kujengewa nyumba ambapo alitoa wito kwa wananchi kuiga mfano wake wa kutoa maeneo yao pale serikali inapotaka kutekeleza miradi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment