NA MWANDISHI WETU, TANGA
WANANCHI
wa Mkoa wa Tanga, hasa wanaojihusisha na kilimo, uvuvi, biashara na
wajasiriamali, wametakiwa kutumia vema fursa zitokanzo na uzinduzi wa
Tawi jipya la Benki ya NMB, Ngamiani, ulioenda sambamba na makabidhiano
ya mabati 250 yenye thamani ya Sh. Milioni 10 kwa Shule ya Msingi
Masiwani, iliyopo Ngamiani, Tanga.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba, akizindua Tawi la
NMB Ngamiani, ambalo ni la 11 mkoani humo, likiwa pia ni tawi la 40
katika Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Arusha na Kilimanjaro),
uliohudhuriwa na Meneja Uchumi na Takwimu wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Arusha, Ernest Ndunguru.
Akizungumza
katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali, wakiwemo
viongozi wa Serikali na vyama vya siasa, Mgumba alisema ufunguzi wa tawi
hilo la 11 mkoani mwake - kati ya matawi 40 kwenye mikoa minne ya Kanda
ya Kaskazini, ni uthibitisho kwamba Tanga inakua kwa kasi kiuchumi na
kibiashara.
“Serikali
inatambua mchango wa sekta za fedha hasa NMB katika kutoa huduma za
kibenki, tunaipongeza NMB kwa jitihada za kusogeza huduma za kibenki kwa
jamii, kwani huduma hizo na sekta ya fedha kwa ujumla, ni kichocheo cha
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.
“Serikali
imeweka mazingira mazuri sana ya kuhakikisha jamii inafikiwa na
inazitumia huduma za kibenki, nashukuru NMB imekuwa ikiunga mkono juhudi
za Serikali katika hili, na hivi karibuni ilitenga Sh. Bil. 200 kwa
ajili ya mikopo nafuu yenye riba asilimia 9 kwenye sekta ya kilimo,”
alisema Mgumba katika hafla hiyo.
Afisa
Mkuu wa Wateja Binafsi na Serikali wa NMB, Alfred Shao, alisema baada
ya Sh. Bilioni 100 za kwanza ilizotenga kukopesha wadau wa kilimo kwa
riba nafuu ya asilimia 10 kwisha, benki yake imeongeza kiasi hicho kwa
kutenga Bil. 100 nyingine kunufaisha kada hiyo muhimu kwa ukuaji wa
uchumi wa Taifa kwa asilimia 9.
Alibainisha
kwamba, NMB Ngamiani linakuwa Tawi la 228 Tanzania kote, ikiwa ni miaka
25 tu tangu ilipoanzishwa (1997), ikiwa na matawi 97 tu na kwamba licha
ya uwingi wa matawi hayo, mashine za kutolea fedha (ATM) 762 na
Mawakala zaidi ya 15,000, lakini benki yake imejikita na kufanya
mapinduzi makubwa kidijitali.
Shao
alifafanua kwamba, wakulima wa mkonge na muhogo, wadau wa sekta hiyo,
pamoja na wafanyabiashara, wafanyakazi na wajasiriamali mkoani Tanga,
wanapaswa kuchangamkia fursa hizo ili kukua kiuchumi na kuimarisha
ukuaji wa benki, hivyo kutanua faida na gawio la Serikali, na asilimia 1
ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Naye
Meneja Uchumi na Takwimu wa BoT, Ernest Ndunguru, aliipongeza NMB kwa
kutambua na kuthamini uwepo wa BoT na kwamba mwaliko waliopewa ni
uthibitisho kwamba wanathamini uwajibikaji wao, hasa ikizingatiwa kwamba
wao ndio wasimamizi wakuu wa sekta ya fedha nchini.
“Uzinduzi
wa NMB Tawi la Ngamiani, ni ishara kwamba NMB iko bega kwa bega na BoT
katika kutekeleza sera za fedha na kuhakikisha mzunguko wa fedha na
huduma za kibenki unawafikia wananchi popote kwa urahisi zaidi, uzinduzi
huu pia ni ishara kwamba NMB inakubalika kwa wananchi kutokana na
shughuli zake,” alisema.
No comments:
Post a Comment