HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 09, 2023

SMZ kufanya mageuzi makubwa kwenye Vyama vya Ushirika

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Vyama vya ushirika vina jukumu kubwa la kuwahamasisha, kuwaunganisha na kuwarahisishia wananchi ili waweze kushiriki katika harakati za kiuchumi, uzalishaji mali na utoaji huduma mbali mbali katika Jamii.


Akihutubia kwa niaba yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Maadhimisho ya siku ya ushirika Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa ya vyama vya Ushirika ikiwemo kuweka mazingira  wezeshi ya Sera, Sheria na Kanuni mbali mbali, hivyo ni wajibu wa Vyama vya ushirika vinavyoanzishwa kuimarisha miamvuli yao ili uwasaidie kufanya na kuratibu shughuli zao kwa maslahi yao na Nchi yetu.

 

Amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha misingi ya haki, uadilifu, demokrasia na utawala wa Sheria vinaimarishwa katika Vyama vya ushirika na kuboresha Maslahi ya wanachama, kusimamia upatikanaji wa mitaji, mafunzo na masomo ili   wanaushirika na wajasiriamali waweze kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ushindani katika soko ambazo zitaleta fursa kubwa  ya kukuza uchumi nchini.

 

Rais Dkt. Mwinyi amezipongea SACCOS zote nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za fedha hasa kwa wananchi wanaoishi vijijini na kueleza kuwa hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua uchumi wa wananchi wake.

 

Pamoja na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametoa wito kwa vijana wanaomaliza masomo katika ngazi tofauti watumie fursa ya kujiunga katika Vyama vya ushirika ili kupeleka maarifa mapya na elimu walioyoipata katika masomo yao ili kuimarisha utendaji na kuchochea ufanisi katika Vyama pamoja na kunufaika na ajira.  

 

Aidha Mhe. Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) imeanzisha mafao ya upotevu wa ajira kwa lengo la kulinda na kumhifadhi Mfanyakazi katika kukabiliana na ugumu wa maisha sambamba na kuwanufaisha wafanyakazi ambao wamepoteza ajira kuanzia Oktoba mwaka 2022.

 

Sambamba na hayo amesema Serikali kwa kuwajali wananchi  wake na kuwawezesha kiuchumi  inajenga kiwanda cha kusarifu zao la mwani litakaposarifiwa Zanzibar litakalokuwa na bei nzuri itakayowasaidia kuongeza kipato cha wakulima na wajasiriamali nchini.     

          

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, kazi, uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudra Ramadhan Soraga ameeleza kuwa Wizara imeanza taratibu za kubadilisha Sheria na Kanuni za Ushirika ambapo siku chache zijazo itaanza kuwashirikisha Wadau vikiwemo Vyama vya Ushirika ili kutoa maoni yao na kupata sheria itakayosaidia kukuza Sekta ya Ushirika nchini.

 

Aidha ameeleza kuwa Tayari Wizara kupitia wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi imeshasaini makubaliano na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) kupunguza zaidi ya  Asilimia 95 za gharama za ubora wa viwango.

 

Akisoma Risala ya Wanaushirika Katibu Mtendaji wa Muungano wa Vyama vya ushirika Zanzibar (CUZA) Bwana Suleiman Ame Mbarouk ameeleza kuwa Sekta ya Ushirika nchini inaendelea kukuwa siku hadi siku ambapo hadi kufikia Juni 2023 Zanzibar vyama vya ushirika vilivyosajiliwa vimefikia Elfu Tatu na Arobaini na Moja (3041)  vyenye Wanachama Hamsini na Moja Elfu, Mia Sita na Hamsini na Sita (51,656).


Awali  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametembelea mabanda ya wanaushirika na wajasiriamali wanaojihusisha na shughuli mbali mbali ambapo amevutiwa na kazi zao kutokana na muamko wao wa kujishughulisha ili kuongeza kipato binafsi na Taifa. raulimbiu ya maadhimisho ya  siku ya ushirika duniani ni "Ushirika ni wadau wa kuhamasisha maendeleo endelevu" .

No comments:

Post a Comment

Pages