September 30, 2023

Makamba: China ni ya kutolewa mfano duniani

Na Selemani Msuya

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba amesema nchi ya China ni ya kutolewa mfano bora kutokana na mchango wake  katika kupunguza umaskini duniani.

Aidha Makamba amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika sekta zote ambazo zitawezesha nchi hizo kupata maendeleo kwa kasi kubwa.

Makamba ameyasema hayo jana usiku wakati wa maadhimisho ya miaka 74 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China ambapo ameweka bayana kuwa uwajibikaji, nidhamu na kujituma ndizo sababu ya nchi hiyo kuendelea.

"Safari ya China kufikia hapa ilipo imechangiwa na viongozi na wananchi wao kujituma na leo hii inasaidia nchi zingine kuendele, ikiwemo Tanzania, tuna la kujifunza ili na sisi tufike huko,"amesema.

Waziri Makamba amesema China imekuwa ikisaidia nchi nyingi duniani kwenye sekta mbalimbali, hivyo ni vema kila nchi kutamani mafanikio hayo.

Alisema kitendo cha China kuwa miongoni mwa nchi zenye nguvu kubwa kiuchumi duniani ni uthibitisho wa ujasiri, dhamira, maono, uongozi, na kufanya kazi kwa bidii na dhamira isiyoyumba.

"Mchango wa serikali ya China katika kupunguza changamoto ya umaskini duniani haupaswi kupuuzwa na kwamba kwa zaidi ya miaka mingi China imetoa mchango mkubwa katika ustawi wa dunia, utulivu na kufufua uchumi wa nchi mbalimbali. Naamini kila anayetaka kujifunza anaweza kufanya kama China,"amesema

Waziri Makamba amesema, maendeleo ya China na watu wake ni hamasa kwetu sote na yanatoa ukumbusho wenye nguvu wa kile kinachoweza kutekelezwa na nchi tunapofanya kazi pamoja kuelekea kutimiza lengo moja.

Amesema, maadhimisho hayo ni fursa ya kutafakari kuimarika kwa uhusiano wa muda mrefu kati ya China na Tanzania katika maeneo mbalimbali.

"Tunaposherehekea kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China,
tunatafakari pia juu ya kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi zetu mbili (China na Tanzania) katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo, uwekezaji, ulinzi, elimu, biashara, utamaduni na miundombinu,"amesema.

Amesema wananchi wa China wanaitambua nchi Tanzania kupitia Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Reli ya Tazara jambo ambao limechangiwa Tanzania kunufaika zaidi kwa miaka ya hivi karibuni.

Waziri Makamba amesema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na diplomasia ambao umekuwa na matunda kwa miaka yote.

Makamba amesema ushirikiano huo umeifanya China mbia mkubwa wa biashara wa Tanzania na mwekezaji kutoka nje, na hivyo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zetu.

Aidha, Makamba Tanzania inaunga mkono kikamilifu mpango kabambe wa Belt and Road Initiative (BRI), ambao umeonesha matokeo chanya kwa nchi husika.

"Mwezi ujao kutakuwa na Jukwaa la Tatu la Ukanda na Barabara kwa Ushirikiano wa Kimataifa litakalofanyika Beijing, Tanzania tutashiriki kwani mpango huu wa BRI utawezesha kuongezeka kwa biashara, kukuza uchumi wetu na kuboresha maisha ya watu wetu," amesema.

Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian akiongea katika maadhimisho hayo amesema, China imeendelea kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Tanzania kwa miaka saba mfululizo ambapo biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola za Kimarekani bilioni 8.31 mwaka 2022.

Balozi Chen amesema, urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania umekuwa ukiendelezwa kizazi hadi kizazi na unaendelea kushamiri na kumpongeza Rais Samia kufuata nyayo za watangulizi wake kuendeleza.

"China na Tanzania tuna uhusiano na ushirikiano wa kuigwa na kutolewa, lakini hali hiyo ipo kwa nchi zote ambazo zinasimamia misingi ya haki za binadamu na amani," amesema.

Balozi amesema mwaka huu pekee, wanafunzi 160 wa Kitanzania wamepata ufadhili wa kusoma nchini China, huku wakiendelea kutoa fursa za mafunzo kwa Tanzania, yanayojumuisha fani mbalimbali kama vile elimu ya ufundi stadi, ujenzi wa miundombinu, kuondoa umaskini na uwezeshaji wa wanawake na hivyo kusaidia nchi kuibua vipaji vya taaluma mbalimbali ambavyo vinahitajika kwa haraka kwa maendeleo ya taifa.

Chen amesema hali ya uchumi wa China ni imara na umekuwa ukiendelea kukua kwa asilimia 5.5 kila mwaka na kufanya pato la Taifa la China kuongezeka zaidi.

"Pato la Taifa la China (GDP) limekuwa likikua kwa asilimia 5.5 mwaka hadi mwaka katika nusu ya kwanza ya 2023, na kufikia Yuan trilioni 59.3 (sawa na USD trilioni 8.24); uagizaji wa bidhaa na mauzo ya nje ulizidi Yuan trilioni 20 (sawa na dola trilioni 2.8) kwa mara ya kwanza," amesisitiza Balozi Chen

Kufuatia kuongezeka kwa GDP pamoja na ukuaji wa uchumi kukukua zaidi, Balozi Chen ameeleza kuwa hatua hizo zimepelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kutabiri kuwa China itachangia asilimia 34.9 katika ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka huu, jambo ambalo lilionesha kikamilifu imani ya ulimwengu katika maendeleo ya ubora wa juu ya China.

Maadhimisho hayo ya 74 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China yamehudhuriwa na kiongozi wa mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed, Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Pinda, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mussa Hassan Zungu, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali, maafisa kutoka serikalini na balozi mbalimbali, wanafunzi.


No comments:

Post a Comment

Pages