Na Selemani Msuya
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa nchini India kuanzia Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu, kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo ameweka wazi kuwa ziara hiyo inaenda kuendeleza ushirikiano wa kijamii, kiuchumi na kihistoria kwa nchi hizo mbili.
Makamba amesema Rais Samia atawasili India Oktoba 8 mwaka huu ambapo atapokewa kwa heshima zote za kiongozi wa nchi na baada ya hapo atakutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika makazi yake na baadaye atakutana na Rais wa India Droupadi Murmu.
Amesema pia Rais Samia atapata nafasi ya kutembelea jumba la makumbusho lenye kaburi la Waziri Mkuu mstaafu wa India Mahatma Ghandhi ambaye ana historia nzuri na Tanzania tangu kipindi cha uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Waziri Makamba amesema India imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta mbalimbali kama afya, kilimo, maji, biashara, uwekezaji na nyingine ambapo kila mwaka kumekuwa na ungezeko la ushirikiano, hivyo ziara hiyo inaenda kuboresha mashirikiano hayo.
"Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu Rais Samia akiwa ameambatana na wasaidizi wake na wadau wengine atakuwa India ambapo ziara hiyo itawezesha kusainiwa makubaliano 15 kati ya nchi hizi mbili, yakihusisha sekta ya viwanda afya, elimu, biashara, maji, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, kilimo na nyingine,"amesema.
Makamba amesema kupitia ziara hiyo Tanzania itanufaika na fursa za mafunzo kwa Watanzania 1,000 na kuvutia wawekezaji katika eneo la kidigitali ambalo India wamepiga hatua.
Amesema pia ziara hiyo inatarajiwa kufanikisha ujenzi wa kituo cha upandikizaji wa figo, kiwanda cha kuzalisha chanzo za binadamu na wanyama na vingine ambavyo vitawezesha sekta hiyo kuwa bora zaidi.
Waziri Makamba amesema katika ziara hiyo ambayo itahusisha wafanyabiashara wa kitanzania takribani 80, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), mafanikio makubwa kwa wadau wa pande zote mbili.
Amesema sekta ya kilimo itanufaika kupitia zaira hiyo ambapo wahusika wataeleza kwa kina kuhusu zao la korosho, mbaazi na choroko ambayo yanapatikana kwa wingi nchini.
Waziri huyu amesema India ni wanunuzi wakubwa wa mazao hayo hasa mbaazi hivyo ziara hiyo itaweza kutangaza kwa wafanyabishara na wawekezaji wa nchi ni hiyo kuja kutumia fursa hiyo.
"Pia tunatarajia ziara hii inaenda kuleta wawekezaji kwenye sekta ya viwanda ambapo wafanyabishara kutoka India wataanzisha Kongani ya Viwanda kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 1,000. Kubwa zaidi tunatarajia wawekezaji kwenye eneo la Karakana ya ujenzi wa meli na vivuko ambavyo vinatumika hapa nchi,"amesema.
Amesema Tanzania imejaliwa fursa ya vyanzo vya maji kama bahari, maziwa na mito mikubwa hivyo ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha usafirishaji kwenye maeneo hayo uwe wa uhakika.
Waziri Makamba amesema pia kupitia zaira hiyo Rais Samia na wenyeji wake watazungumzia mchakato wa awamu ya pili ya Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria ambapo awamu ya kwanza inaelekea mwisho.
Makamba amesema Rais Samia ataweza kukutana na wafanyabishara kwa makundi na mmoja mmoja ambapo atawaeleza fursa zilizopo nchini ili waweze kuja kuwekeza.
October 05, 2023
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.



No comments:
Post a Comment