January 29, 2013

Benki ya Exim yafungua tawi la pili Mkoani Kilimanjaro


DAR ES SALAAM, Tanzania

BENKI ya Exim, imeendeleza mpango wake wakufikia wananchi wengi nchini kwa kufungua tawi la pili mkoani Kilimanjaro na kufikisha idadi ya matawi 25 kwa jumla nchi nzima.

Tawi hilo jipya, lililopo Moshi mjini, limekamilika na lipo tayari kutoa huduma bora za kibenki kwa jamii iliyopo ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro wakati benki hiyo ikijiimarisha katika sekta ya kibenki nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi hilo jipya mjini Moshi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Bw. Anthony Grant alisema kuwa ufunguzi wa tawi hilo jipya unaonyesha dhahiri jitihada za benki yake kuhakikisha kuwa watanzania wengi wanapata huduma za kibenki katika gharama nafuu.

Grant alisema kuwa benki yake imejikita katika mpango madhubuti wa kutanua huduma zake wenye lengo la kuhakikisha kuwa benki inafungua matawi mapya katika maeneo ambayo hayajafikiwa na benki nyingine.

“Utekelezaji wa mpango huo sasa upo katika hatua za mwisho. Tumejipanga kufungua matawi mapya matano zaidi mwaka huu ikiwa ni katika jitihada zetu za kusogeza huduma zetu karibu na wananchi hususani vijijini,” alisema Grant.

Alisema kuwa uzinduzi wa tawi hilo mkoani Kilimanjaro unadhihirisha dhamira kubwa ya benki kuhakikisha watu wote katika mkoa huo wanapata huduma za kibenki.

“Ni matumaini yangu kuwa tawi hili jipya litasaidia kukuza uchumi kwa wakazi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Tuna matumaini ya kufungua matawi zaidi mkoani Shinyanga, Tabora, Arusha na Dar es Salaam kabla ya mwisho wa mwaka,” alisema Grant.

Grant alibainisha kuwa licha ya uwekezaji wa benki katika maendeleo ya kiuchumi nchini, haitakata tamaa katika jitihada zake za kuhakikisha inakuza wafanyabiashara wadogo na wakati nchini.

 “Tunatazama maendeleo ya Tanzania ya siku za usoni katika mtazamo ulio chanya na tutaendelea kuiunga mkono serikali katika agenda yake ya maendeleo, tukijitahidi kutoa fursa zaidi za shughuli za kiuchumi na uzalishaji,” aliongeza Grant.

Kwa upande wake Meneja wa Tawi hilo jipya la Moshi Paul Mbanga wakati wa tukio hilo alisema kuwa benki yake imejizatiti katika kuchangia kikamilifu maendeleo ya sekta ya fedha nchini.

“Ni matumaini yangu kuwa tawi letu jipya tulilozindua litasaidia kuweka uwiano kati ya faida inayopata benki na huduma nzuri za kibenki katika jamii zilizopo mkoani Kilimanjaro,” alisema.

Aidha Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Leonidas Gama aliwaasa wananchi wa mkoani Kilimanjaro kutumia fursa zitakazojitokeza baada ya uzinduzi wa tawi hilo jipya kwa faida yao.

“Kwa wakati huu, kuhifadhi fedha katika vibubu au chini ya mito, si njia ya kizamani pekee bali pia ni njia isiyo salama.

Nawashauri kuweka fedha zenu benki ilimpate viwango vizuri vya riba ili kuongeza thamani ya fedha zenu. Nawaasa kuwa na utamaduni wa uwekaji akiba si tu utakusaidia kuboresha maisha yenu lakini  pia kukuza maendeleo ya uchumi kwa ujumla,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment

Pages