January 17, 2013

Choki kupagawisha Garden Breeze Jumapili


Na Mwandshi Wetu

BAADA ya makamuzi aliyoyafanya wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Garden Breeze, mkali wa muziki wa dansi nchini, Ali Choki ‘Mzee wa Kibaha,' Jumapili hii atarejea tena katika viunga hivyo vilivyoko Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam kuwakimbiza.

Choki akiwa na bendi yake ya Extra Bongo Next Level, ‘Wazee wa Kizigo’ sambamba na mkali mwingine wa muziki huo nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’, alidihirisha uwezo wake mkubwa wa uimbaji na kukonga vema nyoyo za mashabiki waliomba marejeo hayo.

Akizungumzia shoo ya Jumapili hii, Choki alisema, bendi yake imepania kuhakikisha inakonga nyoyo za mashabiki wao wa Magomeni na maeneo ya jirani na kwamba, kila atakayehudhuria atakubaliana na hilo.

“Kazi zetu zinatambulika, watakaokuja watashuhudia shoo kali kutoka kwa wanamuziki na wanenguaji mahiri wa dansi. Waje kwa wingi na kila atakayeingia Garden Breeze, hatojutia uamuzi wake wa kuja kujinafasi nasi wana wa ‘Next Level’ wikiendi hii,” alitamba Choki.

Aidha, mkongwe wa dansi Afrika Mashariki na Kati, Tshimanga Kalala Asosa, naye atafanya vitu adimu akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz, watakapotumbuiza kwenye ‘kijiji hicho cha maraha’ cha Garden Breeze leo usiku.

Asosa maarufu kama ‘Mtoto Mzuri’, alisema, amejiandaa kukonga nyoyo za mashabiki kwa vibao vyake vipya na vya zamani, vikiwamo vile vilivyompa umaarufu mkubwa, kiasi cha kuitwa hapa nchini kuanzisha bendi kongwe ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ mwaka 1978.

“Nitawapa mashabiki vitu vipya na vile vyote nilivyopata kuimba katika bendi zangu tangu nikiwa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), hadi hapa Bongo,” alisisitiza Assosa bila kutaja nyimbo hizo na kuwataka mashabiki wa muziki wa dansi kufurika Garden Breeze.

No comments:

Post a Comment

Pages