January 03, 2013

Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji


Na Zitto Kabwe
'Dar inachangia asilimia 80 ya mapato. Kitovu cha Uchumi. Dar inachangia 90% ya ufisadi. Uti wa mgongo wa ufisadi nchini'
Malumbano kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri wa nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni dalili ya Serikali kuweweseka.
Katika kauli ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari, Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yetu.
Moja, Serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa kupitia zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector study 2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010). Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu. Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni  (sawa ni shilingi trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50 nyuma kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao la Korosho miaka nenda miaka rudi?
Pili, Serikali imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel, Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa ‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika kulinda uhuru wa Taifa letu?
Tatu, Serikali inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio inazalisha asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni aibu Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi Ofisi zao Kuu zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi.Hata hivyo inawezekana kuwa ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya mapato ya nchi. Basi na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya ufisadi wote nchini. Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es Salaam na fedha nyingi za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.
Mwisho, maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi. Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo. Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani 76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Kampuni ya Resolute ya Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14,  Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3 bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola 11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?
Pia watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?
Uwajibikaji katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.

No comments:

Post a Comment

Pages