January 15, 2013

TABOA KUWACHONGEA WAMILIKI WA MABASI SUMATRA



DAR ES SALAAM, Tanzania.

UMOJA  wa Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) umeahidi ‘kuwachongea’ baadhi ya wamiliki wa mabasi katika Ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kwa kukaidi taratibu za uendeshaji wa mabasi yao.

Aidha umesikitishwa na ajali za mabasi zilizotokea juzi huku uliomba Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kuchunguza kwa makini juu ya tukio hilo kisha kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha ajali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, amesema kuwa pamoja na Serikali kuonyesha nia ya kuondoa matatizo yaliyopo katika sekta ya usafiri, wapo baadhi ya wamiliki wenye nia ya kuhujumu mikakati iliyopo.

Aliongeza kuwa  wapo baadhi ya wamiliki wa mabasi wamekuwa wakienda kinyume na utaratibu huo kwa matakwa yao binafsi jambo alilosema kuwa linakiuka maagizo yaliyowekwa.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuwa sasa ipo karibu na sisi katika hatua mbalimbali, ushirikiano huu umeonyesha wazi kuwa mbeleni utakuja kuzaa matunda ambayo dalili zake hivi sasa tumeziona isipokuwa wapo baadhi ya wenzetu wanakwenda kinyume na yale tunayokubaliana” alisema Mrutu.

Mrutu alisema pamoja na mikakati mizuri iliyofanywa na  Serikali kwa kuweka utaratibu wa ratiba za  mabasi, baadhi ya wamiliki wakekuwa wakiendesha safari kwa utaratibu wao na hivyo kuleta hofu ya kutokea kwa ajali alizodai kuwa nyingi zinasababishwa na uzembe pamoja na kutofuata ratiba.

“Juzi tulikuwa na kikao na Kamati ya Bunge, moja ya mambo tuliyokubaliana ni kufuata ushauri tunaokubalaiana na Serikali, huu ndio ushirikiano ambao kama kweli tuna nia ya kuendeleza sekta ya usafiri nchini, hatuna budi kuufuata” alisema Mrutu.

Mrutu alisema kutokana na uwepo wenzao wanaokwenda kinyume na makubaliano hayo, wameamua kuunda kamati itakayokuwa ikifanya kazi katika njia kuu tano za mabasi kutokea Dar es salaam, kwa lengo la kuwafuatilia wale wanaokwenda kinyume na utaratibu huo na ili baadae wakafikishe matatizo yao Sumatra pamoja na Polisi makao makuu ya Usalama barabarani.

Alizitaja njia nne zitakazofuatiliwa na kamati hiyo ya watu watano kuwa ni pamoja barabara ya Dar es salaam kwenda Arusha, Dar es salaam kwenda Mwanza, Dar es salaam kwenda Mbeya, pamoja na Dar es salaam kwenda Mikoa ya Kusini.

Akizungumzia tukio la ajali iliyotokea juzi na kupoteza maisha ya watu saba, Mrutu alisema kinachoonekana ni kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa madereva, hivyo ni vyema jeshi la Polisi likafanya uchunguzi wake wa kina na kuwachukulia hatua kali wahusika.

No comments:

Post a Comment

Pages