January 25, 2013

TANZANIA NA JAPAN ZASAINI MKATABA WA BILIONI 28.2



DAR ES SALAAM, Tanzania

WAZIRI wa Fedha, William Mgimwa, amesaini mkataba wa sh. Bilioni 28.2 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya miradi mitatu ya kiuchumi na kijamii.

Serikali ya Japan itafadhili miradi hiyo kupitia Shirika lake la ushirikiano wa Kimataifa (JICA).

Akizungumza jana jijini Dar Es Salaam, Mgimwa alitaja miradi hiyo kuwa ni upanuzi wa barabara ya Kilwa ili watu kuweza kufika kwa wepesi katikati ya mji na eneo la bandari.

Mgimwa alisema kuwa mradi huo utakuwa wa kilometa 1.3 na utaanzia eneo la Gerezani linalokutana na Kamata mpaka barabara ya Kilwa ujenzi utakaosababisha barabara hizo kuwa nne tofauti na sasa ambapo zipo mbili na mradi huo utagharimu sh. Bilioni 20.

Pia alisema kuwa mradi wa pili ni kubuni na kujenga barabara za juu (flyover) ilikuondoa foleni katika barabara ya Mandela na Nyerere ikiwemo kujenga daraja eneo la Tazara mradi ambao utagharimu sh. Bilioni 1.26.

Alisema kuwa mradi wa tatu utahakikisha tatizo la ukosefu wa chakula linakwisha hasa katika mikoa yenye uhaba.

“Mradi wa tatu utahakikisha usalama wa chakula na mradi huu unalengo la kutimiza sera ya kilimo kwanza na kutoa nafasi ya kuzalisha kwa wingi na kujenga usalama wa chakula kwa watu wenye hali ya chini mradi ambao utagharimu sh. Bilioni 6.92” alisema Mgimwa.

Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, alisema kuwa nchi ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuitaka Serikali kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa mradi husika ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages