January 09, 2013

WADAU WA SOKA WAKIPONDA KIKOSI BORA CHA FIFA 2012

Kikosi Bora cha Mwaka 2012 ‘FIFA/FIFPro World XI,’ kutoka kushoto waliosimama nyuma ni Ronaldo, Marcelo, Ramos, Pique, Alves, Casillas, wakati waliosimama mbele ni Falcao, Messi, Iniesta, Xavi na Alonso. Kikosi hicho kilitangzwa juzi usiku wakati wa hafla ya kumtunukia Mwanasoka Bora wa Mwaka ‘Ballon D’Or’ iliyonyakuliwa na Lionel Messi.

LONDON, England

Wakali wanaounda kikosi hicho ni: Iker Casillas, Dani Alves, Gerard Pique, Sergio Ramos, Marcelo, Xabi Alonso, Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Cristiano Ronaldo, Radamel Falcao na Lionel Messi

BEKI wa kimataifa wa England, Ashley Cole amelipiga kijembe Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa kusema anahitaji kuwa na pasi ya kusafiria ya Hispania, ili aweze kutambuliwa kuwa ni beki bora wa kushoto duniani kwa sasa.

Kauli ya mshindi huyo wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, umetokana na kutoingia kwake yeye ama nyota yeyote wa Chelsea katika Kikosi Bora cha Mwaka ‘FIFPro World XI 2012’ kilichotangzwa juzi huko Zurich, Uswisi.

Kama hiyo haitoshi, Ligi Kuu ya England haikutoa mchezaji hata mmoja miongoni mwa wakali 11 waliotangazwa kuwamo kikosini, huku wote wakitoka katika Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ – 10 kati yao wakitoka klabu za Real Madrid na Barcelona.

Sita miongoni mwa nyota hao 11 wanaounda kikosi hicho bora wakiwa ni walioiwezesha Hispania kutwaa ubingwa wa Mataifa Ulaya Euro 2012.

Wachezaji walioingia katika kikosi hicho ni: Iker Casillas, Dani Alves, Gerard Pique, Sergio Ramos, Marcelo, Xabi Alonso, Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Cristiano Ronaldo, Radamel Falcao na Lionel Messi.

Katika mjadala mpana kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, mshambuliaji wa Barnet, Steve Kabba alikosoa kutokuwapo kwa Cole kikosini, lakini nyota huyo wa England akajibu: “Hakuna utani kinachotokea hapa kinashangaza. #Nahitaji pasi ya kusafiria ya Hispania.”

Mchangiaji mwingine na nyota wa zamani Stamford Bridge, nguli Ron ‘Chopper’ Harris alisema: “Inashangaza sana kuona timu iliyotwaa ubingwa wa Ulaya haijaingiza mchezaji hata mmoja katika kikosi bora cha mwaka cha Fifa.

“Achana na mfumo huo uliotumika – kama nitaambiwa nichague kati ya Marcelo na Ashley Cole, sitomchagua Marcelo. Lakini pia kuna mameneja bora Ulaya, akiwamo Jose Mourinho!”

Mzozo wa ubaguzi baina ya John Tery na Anthon Ferdinand, ulimsukuma beki wa Manchester United, Rio Ferdinand kutomuunga mkono Cole kuwamo kikosini, baada ya nyota huyo ‘mweusi’ kumtetea Terry katika sakata hilo.

Badala yake Ferdinand akachangia kwa kushangaa kutoingia hapo kwa mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie, aliyekuwa akichezea Arsenal. Akaandika: “Kwa vipi Van Persie hayumo katika kikosi hicho?”

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Lothar Matthaus alichangia kwa kuandika: “Sielewi kama hiki kikosi cha FIFPro World XI, kinatakiwa kuhusisha nyota wa La Liga tu.”

Harris naye akaongeza: “Watu wengi duniani wanasema Ligi Kuu ya Hispania ni bora zaidi duniani. Lakini kama ukiziweka kando Barcelona na Real Madrid, kipi kingine kilichomo humo?”

Miongoni mwa wakosoaji wa kikosi hicho walishangazwa na kutowamo kikosini kwa kiungo wa kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo, kiungo mahiri aliyefanya mambo makubwa na kuiwezesha Juventus kutwaa Serie A na kuifikisha Azzurri fainali ya Euro 2012.

No comments:

Post a Comment

Pages