April 01, 2013

RAMBIRAMBI MSIBA WA BEHEWA SEMBWANA


Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union, TPC na Taifa Stars, Behewa Ali Sembwana (72) kilichotokea jana usiku (Machi 31 mwaka huu) mkoani Tanga.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

Sembwana aliyekuwa akicheza wingi ya kulia alidumu katika Taifa Stars kwa miaka kumi, kama ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars) aliyoiwakilisha katika michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Sembwana, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 1 mwaka huu) kijijini kwake Lusanga, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina

WALIBERIA WA AZAM KUWASILI KESHO
Timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia inatarajia kuwasili nchini kesho (Aprili 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam itakayochezwa Jumamosi (Aprili 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Young Controllers itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.

Msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 37 wakiwemo wachezaji 21 na utaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo Robert Alvin Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.

Wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy, Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.

Benchi la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu Robert Lartey akisaidiwa na Samuel Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel Massaquoi.

Timu hiyo inatarajia kundoka kurejea Monrovia, Aprili 8 mwaka huu kupitia Nairobi, Kenya saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI WA POLISI TABORA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa ajali ya pikipiki mjini Tabora.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1 mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali pema peponi. Amina


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages