September 12, 2013

Mgogoro wa Wakulima na Wafugaji Mvomero ni Mtaji kwa Viongozi na wanasiasa!

Na Bryceson Mathias
MGOGORO wa Wakulima na Wafugaji wa wilaya ya Mvomero, mbali ya kuathiri mazao na kuwasababisha Njaa wakazi hao, sasa umekuwa kama ni Mtaji wa Viongozi na Wanasiasa wilayani humo.
Sababu zinazoakisi Mgogoro huo kuwa ni pamoja na Matamko na Maagizo yanayotamkwa na Serikali kuwa ya Majadiliano zaidi badala ya kutumia Sheria, jambo ambalo sheria zisipotumika, kunasababisha kutokea maafa na vifo vya kutisha kutokana na kuzoea amri.
Migogoro hii si ya Juzi wala jana, bali imekuwepo kwa muda mrefu wilayani Mvomero, ikiwemo wilaya ya Kilosa eneo la Mabwegere, ambapo watu zaidi ya wanne walipoteza maisha kutokana na mapigano yaliyoibuka baina yao wakigombea ardhi.
Kinachonishangaza ni uoni hafifu wa Viongozi wa Serikali na kisiasa kuhusu kile kinachoweza kutokea mbeleni iwapo matamko na Amri zao kila mara zinapelekea kurudiarudia kwa Migorogoro hiyo.
Inaonesha na kuthibitishwa kuwa uwajibikaji na utendaji wao kuhusu adha hiyo, umekuwa hauna mashiko zaidi ya kuwepo kwa mwanya wa watendaji hao, kupelekea kujinufaisha wenyewe kupitia mgongo wa Mgogoro huo, wakitumia uelewa mdogo wa waathirika.
Wafugaji na wakulima wanaoathirika na Migogoro hiyo kifedha na kimazao, kila mara wamewalalamikia viongozi hao kuwa, Migogoro hiyo imekuwa haipewi utatuzi wa kudumu kwa sababu miongoni mwa viongozi na wanasiasa hao wanafaidika na kuwepo kwake.
Imetuhumika kwamba, pindi mifugo ya wafugaji inapokamatwa ikiharibu mazao ya wakulima! Ili kutoa na nafuu ya Mgororo ulio mbele, baadhi ya viongozi hao (hawakutajwa) hupewa Ng’ombe na Pesa za kutosha kama kitu kidogo na Wafugaji, hivyo kesi zao kufumbwafumbwa.
Kutokana na Wakulima kukosa Nguvu ya kifedha kupambana nao, hujikuta wakibaki Maskini wa kutupwa kutokana na mazao yao kuliwa kwa nyenzo ya Mchezo huo Mchafu, unaodaiwa kufanywa kuanzia kwa baadhi ya Wenyeviti na watendaji wao wa Vitongoji, Vjiji, Kata, Tarafa, Wilaya hadi mkoani.
Uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya Wafugaji na Wakulima kwa upande wao, wamevitupia Lawama na kuvituhumu Vyombo vya Dola wakidai kwamba wako baadhi yao wamekuwa wakiwapatia Mifugo kama kitu kidogo ili kuwatetea, na mifugo hiyo wanawafugia.
Walipoombwa wawataje baadhi ya Askari, Viongozi na Wanasiasa wanaojihusisha na Unyafunyafu huo wa Kiuongozi,  wafugaji hao walisema kwa lugha isiyo sahihi,
“Mwandisi, sisi haiwezi kuwataja mtu hiyo kwa sababu ni kama Fimbo, Kisu Guso yetu inatutulinda kwa keso” alisema mmoja wao.
Aliongeza kusema, Wao wanashangaa kukamatwa na kulipishwa faini kuwa, kwa sababu Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji, Kata na baadhi ya Wanasiasa, ndio huwatafutia watu wenye Mashamba yenye Mabua ambapo huwauzia Sh. 10,000/- kwa Eka ili walishe Ng’ombe baada ya wao kuwapa kitu kidogo.
Alisema wanapopeleka Mifugo kwenda kwenye eneo lenye Mabua, ndipo huzidiwa nguvu na Ng’ombe zilizoona Majani Mabichi (Mazao) kwenye Mashamba ya watu wengine ambayo bado hajaiva au kuvunwa, ambapo walidai wao huona kama ni Majani na chakula cha Ngo’mbe zao.
Hivi karibuni baada ya Wafugaji kuingiza mifugo kwenye Mashamba ya wakulima katika Kijiji cha Kisala Kata ya Sungaji na Ng’ombe hao kula Eka tatu za Mahindi ya, Alex Kazimheza, kwa hasira wakulima walikatakata Mapanga Ngombe zaidi ya 15 na kuwa Vibutu.
Hasira hizo zilizusha wakulima kuandamana na kufunga barabara ya Mvomero Handeni huku Magari ya Abiria na Usafirishaji wa Mizigo ilikwama kwa saa kadhaa toka saa 4 asuhuhi hadi saa 11 walipotawanywa kwa Mabomuna na Kikosi cha kuzuia Fujo (FFU).
Baada ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero katika Kikao cha maridhiano baina ya Wafugaji na Wakulima, alitoa amri wafugaji wote waliovamia na kuhamia na Mifugo wilayani humo wahame ndani ya siku saba kwa hiari yao na siku 14 watahamishwa kwa Nguvu.
Siku hizo ambazo zilikwisha 6.9.2013 na kutakiwa zifuatiwe na kuondolewa kwa Nguvu, juzi 9.9.zilikanyagwa na wafugaji hao walioingiza tena mashambani mwa wakulima Ng’ombe zaidi ya 1,000 ambapo wakulima ambao sasa wamechukuwa mafunzo ya ulinzi kupambana na Wafugaji waliwakamata.
Hapo ndipo ninapoona udhaifu wa Viongozi Serikali na wanasiasa kuua Tembo kwa ubua, ambapo husuluhisha Migogoro kwa kutumia Siasa badala ya Sheria na kutoa maangalizo ya Sheria, ilihali amri hizo zinapuuzwa na kuonekana utatuzi wa Migogoro hiyo ni kama Mchezo wa kuigiza na si uwajibikaji.
Hali inayofanywa na Viongozi hao na wanasiasa kuwahadaa wananchi kwa matamko  yaiyotekelezeka, yanaweka chuki miongoni mwao hasa pale ambapo anayefanya uharibifu wa kuharibu mazao au kuangamiza Ng’ombe analipishwa fedha kiduchu ukilinganisha na gharama za kilimo, hivyo kufikia kulipizana visasi.
Mfano Ng’ombe 1,000 waliokamatwa na walinzi wa Sungusungu ya wakulima wakila mazao kijiji cha Kisala 9.9.2013 ikiwa ni ndani ya siku 14 za wafugaji kuhamishwa kwa Nguvu, badala ya kulipishwa Sh. 50,000/- kila Ng’ombe kama ilivyoridhiwa, walilipishwa 10,000/-.
Viongozi walibadilisha makubaliano ya awali na kuwatoza kila Ng’ombe 10,000/- ambapo ukipima na uharibifu uliofanyika shambani fedha hizo hazilipi gharama husika, hivyo kuwepo kutoridhika miongoni mwao kati ya Mtenda kosa na mtendewa.
Jambo kama hili bila kutumia Sheria, badala yake wanasia na Viongozi hao wanatumia mazungumzo yanayokiuka Sheria na kitu kidodgo, yanalimbika Hasira na visasi baina ya Mkulima na Mfugajiji kila mmoja kwa maumivu yake, jambo ambalo baadaye husababisha  kuibua  maafa na Vifo.
Aidha niseme, inawezekana Viongozi wa Dola na siasa wilayani mvomero wamekaa muda mrefu na kuzoeleka na wafugaji kiasi kuona wanakaa na babu hivyo kufanga mambo mengi ndivyo sivyo ambayo hayawezi kuthibitiwa kutokana na kuwa na maslahi binafsi au kulindana.
Hivyo ni budi viongozi hao wakafumuliwa kwa kuahamishwa ili kusuka upya viongozi wasiolalamikiwa kwa tafsri ya kutuhumiwa kupokea rushwa za mifugo na fedha, na kuendeleza misuguano inayoweza kuepukika na isiyo na tija, ila kusababisha Umaskini na Njaa.
Uthibitisho wa kutokuwepo uwajibikaji, ni kujirudiarudia kwa migogoro na vurugu hizo kila mara, ambapo viongozi wa Dola, Serikali na kiasi, kushindwa kulipatia ufumbuzi huku wananchi hao wakijeruhiana na kuuana pasipo na sababu.
nyeregete@yahoo.co.uk 07159933308.

1 comment:

  1. Nakushukuru sana Bryson Mathias, kwa kufuatilia migogoro ya wakulima na wafugaji mvomero na kilosa. Tatizo hili linaweza kumalizwa ikiwa tu uongozi wa dola kwa kushirikiana na Halmashauri husika kutuma timu za wataalam ambao wataandaa madodoso ili kudadavua maoni na mapendekezo kutoka kwa waathirika wa pande mbili za mgogoro kwani kila upande utaweka bayana nini hawakipendi na kipi wangependa kifanyike ili kumaliza migogoro.a sheria peke yake bila ya uelewa wa sheria zenyewe kutokana na wakulima na wafugaji hawa hawako acces na taarifa mbalimbali za kijamii kutokana na jinsi mazingira yanayowazunguka kuwagawa-chukulia mfugaji maisha yake yeye na ng'ombe,ng'ombe na yeye polini, ni lini atajua mahusiano na watu wa shughuli zingine katika jamii?
    joune2000@gmail.com 0787032679

    ReplyDelete

Pages