September 13, 2013

Rais Kikwete; Kataa Kusaini Muswada uliosababisha Ngumi bungeni!

Na Bryceson Mathias
 
PAMOJA na kwamba Rais Jakaya Kikwete anakabiliwa na wakati mgumu kuamua kama atasaini au kukataa  kusaini sheria ya muswada wa kuandika katiba mpya, ni rai yangu alitake bunge litimize kwanza hitaji lililoleta sokomoko na kusababisha wabunge watwangane.
 
Kikwete akifanya hivyo, atakuwa ametumia busara na hekima ya Mfalme Sulemani pale alipowaamua akina wa mama wawili walipogombea mtoto mzima, kila mmoja akimkataa mtoto aliyekufa akisema si wake ila ni wa mwenzake na yeye amefanyiwa hila.
 
Kisa chenyewe kikilikuwa hivi;- Wanawake wawili, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, “Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.
 
“Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia.
 
“Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.

“Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa”. Inasema Biblia katika Kitabu cha kwanza cha Wafalme 3:17-21.
 
Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.

Ndipo mfalme akasema, .. Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.
 
Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.  Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.
 
Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema,
 
“Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe”.. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake. 1 Wafalme 3:22-27.
 
 Kwa kuwa Kikwete anawaongoza watanzania wote, kama akikataa kusaini ataifanya Kamati ya Uongozi ya Bunge ijadili Makandokando yote ambayo yalikuwa yametokea juu ya muswada huo, ukiwamo uongo au ukweli wa Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, na uongo au ukweli wa Serikali bungeni na masuala mengine yote.
 
Kuwa kufanya hivyo Kikwete atalifanya Bunge lipate mwelekeo chanya juu ya muswada huo na kutoa Taswira nzuri kwa mchakato mzima wa Katiba Mpya ili iwe ni kwa masilahi ya wananchi wa Tanzania si kwa ajili ya Chama fulani au watu binafsi kwa manufaa yao.
 
Busara na hekima hiyo ya Kikwete, haitakuwa ngeni ila itafanana na ile aliyowahi kutumia awali, ambapo kutakuwa na uwezekano mkubwa muswada huo ukarejeshwa bungeni ili ujadiliwe baada ya kutimiza vigezo.
 
Nina Uhakika Kikwete anaweza kuruka kikwazo kama alivyofanya Sulemani kwa wanawake wale wawili iwapo atapokea ushauri wa Wahenga wa Maandiko Matakatifu kama yalivyoandikwa katika Biblia Luka 16:13 kwamba,
 
 "Hakuna Mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja nakumdharau mwingine. Asikipendeze Chama cha Mapinduzi (CCM) au Wapinzani ila Mustakabali wa Watanzania”.  
 
Hivyo ni wakati muafaka kwa Rais Kikwete katika Mchakato wa Katiba Mpya hii, asikubali kuwapendezesha CCM kama Chama chake wala Wapinzani wanaowakosoa CCM, bali awapendelee watanzania na kizazi cha Tanzania cha baada ya 2015cha kesho, kesho kutwa na mtondogoo!.
 
 Ni rai yangu Kikwete asiwe na ugumu huo, ambao pengine utatokana na dhamira yake   kwamba anataka kuweka historia ya kuandika Katiba upya wakati baadhi ya viongozi wasiolitakiwa Mema Taifa letu wanazunguka kufanya njama za kisirisiri, kuhujumu mchakato wa Katiba Mpya kama njia ya kumkomoa Rais Kikwete.
 
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308

No comments:

Post a Comment

Pages