September 17, 2013

SUNDAY KAYUNI KUHUDHURIA KOZI YA WAKUFUNZI WA CAF CAMEROON

MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni

DAR ES SALAAM, Tanzania

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu, ikiwamo pia kuwapa ‘methodolojia’ mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi zao

MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni ameteuliwa kushiriki Warsha ya Wakufunzi wa Makocha wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), itakayofanyika kuanzia Oktoba 22 hadi 24 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon, ikishirikisha wakufunzi 18 wa CAF.

Wambura alibainisha kuwa, madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu, ikiwamo pia kuwapa ‘methodolojia’ mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi zao.

Mbali ya Kayuni wa Tanzania, wakufunzi wengine kwa mujibu wa taarifa ya CAF kwa TFF ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana) na Fathi Nossir (Misri).

Wengine ni Faouzy Altaisha (Sudan), Fran Hilton Smith (Afrika Kusini), Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Shelisheli).

No comments:

Post a Comment

Pages