September 12, 2013

UNYAMA HUU WA DC ISAAC WA KONDOA UNAKUBALIKA ZAMA HIZI ZA UHURU?

Na Bryceson Mathias

HIVI karibuni, Mkuu wa Wilaya Mpya ya Chemba Kondoa, Francis Isaac, ametuhumiwa kuagiza Viongozi 19 wa kijiji cha Songambele warushwe kichura na kuvuliwa nguo kwa kushindwa kufyatua tofali za ujenzi wa Sekondari, kabla kurundikwa kituo cha Polisi.

Tukio hilo limekuja tukiwa bado tukikumbuka  ubabe na unyama wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali, aliyeamuru walimu 16 wacharazwe viboko kwa kile alichodai ni utoro na uchelewaji wao wa kufika shuleni.

Wakati Mnali alipoulizwa kuhusu kuwachapa bakora walimu, alikiri tukio kufanyika na kusema hiyo ni sehemu ya haki yao walimu hao wazembe waliochangia wilaya hiyo kuibuka na matokeo mabaya katika mtihani wa darasa la saba wa mwaka huo, Isaac andai wamekataa kuchangia Maendeleo kwa faida yao.

Kutokana na Agizo la Isaac, Shughuli za maendeleo katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Msada, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma zilisimama baada ya viongozi wake wote kukamatwa na kuwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Kondoa.

Viongozi hao wa Kijiji wanalalamika kwamba, hatua ya kurushwa kichura na baadaye kuvuliwa nguo kabla ya kuingizwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Kondoa, kimewadhalilisha na kuwavunjia heshima mbele ya jamii, hivyo wanataka Isaac awajibishwe.

Wanakijiji akiwemo Mwenyeekiti wa kijiji, Awalu Kishera, alidai Isaac aliwaagiza viongozi hao kufyatua matofali yatakayotosha kujenga madarasa pamoja na mabweni na kwamba mwananchi atakayeshindwa atozwe sh 50,000 kama fidia, jambo ambalo wananchi wameshindwa kutokana na ukame na uhaba wa maji kijijini hapo.

Aliongeza sababu ya pili ya zoezi hilo kushindikana lilitokana na upande wa kilimo ambao hawakufanikiw, ndiyo maana hapakuwa na mwananchi mwenye fedha, na walipomuomba aahirishe hadi mwakani wajiandae mvua zikiwa zimenyesha alikataa.

“Ajabu DC Isaac hakutaka kutusikiliza, aliagiza askari tukaja tukamatwa na kuwekwa mahabusu kuanzia Septemba 3 hadi 5, mwaka huu, na tulipofikishwa mahakamani tulitakiwa kutoa sh 150,000 kama dhamana iwapo huna mdhamini,” alisema Kishera.

Idrissa Omary, ni Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Msada Kondoa alishangazwa na hatua ya Mkuu wa Wilaya kutoa maagizo badala ya kutumia mbinu shirikishi ili kuwasaidia wananchi kutokana na Umaskini walio nao ikiwemo Ukame na Ukosefu wa Maji.

Ingawa baada ya kuhojiwa DC Isaac alikanusha Suala la kuagiza wadhalilishwe na kuvuliwa nguo kuwa si la kweli, akidai halikuwapo na wala hakuagiza hivyo ila suala hilo ni uzushi unaolenga kumchafua kutokana na kufuatlia shughuli za Maendeleo bado watu wamekosa imani nae.

Ni kweli Tanzania ni nchi huru iliyopata Uhuru wake 1961, Jamhuri 1962 na Muungano 1964 baada kuwafukuza wakoloni waliowanyosha watanzania kiasi cha Mwalimu Julius Nyerere kusema, Tumenyonywa kiasi cha kutosha, Tumepuuzwa kiasi cha kutosha na kwamba Unyonge wetu ndio uliotufikisha hapo.

Je hivi nchini bado wapo viongozi wenye nyadhifa kama Isaac ambao bado wanawafanya watanzania watumwa katika ardhi na nchi yao? Hivi bado Ukoloni Mamboleo na Ukoloni Mkongwe, na Ukoloni Gandamizi ungali kwa Viongozi wetu walioaminiwa na Wananchi na Rais?

Je, tabia hizi za baadhi ya Viongozi wasiowaadilifu sizo zile zinazosababisha Wananchi wachoshwe na kuichukia Serikali yao? Je kwa hili nalo tutawasingizia wapinzani kuwa wanawachochea ili nchi isitawalike?

4 comments:

  1. hicho walichokipata ndo wanastahili kwa uzembe waloufanya. Watanzania bana mna visa kweli, mtu akitenda kazi mnasema, akikaa tu napo mnasema so which is which? Najua ndugu mwandishi umetawaliwa na hisia za kisiasa ila unatakiwa kufaham kuwa HAKI HUENDA NA WAJIBU, utapata vipi haki yako kama huwajibiki!?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hongera dc hiyo ndo posho stahili ya wazembe,wavivu na wapika majungu!warudi kufanya kazi sio kukimbilia magazetini ALUTA CONTINUE!!!

      Delete
    2. Heko dc dozi uliyotoa songambele uilete pia changamka Rais amekupa rungu ulitumie usijali viherehere wanaokimbilia magazetini UTENDAJI MBELE MAJUNGU NYUMA!!!

      Delete
  2. ISaack moto ni huo huo mwanzo mwisho,hiyo ndo posho wanayostili wavivu,wazembe na wapika majungu,if u think education is high expensive try ignorance!!!zedycom

    ReplyDelete

Pages