September 23, 2013

Wanasiasa wanaotoa tambo kwenye Majukwaa, wote wana Uchungu na Nchi hii?

Na Bryceson Mathias
NAKUMBUKA usemi wa Babu alisema hivi, ‘Mkulima mmoja Mcha Mungu alitoka Shambani! Ghafla akakutana na Simba. 
Mkulima akashindwa kukimbia akapiga Magoti akaanza kusali huku amefumba macho, alipofumbua akaona Simba naye  amepiga Magoti anasali’.
Mkulima alimuuliza Simba; Na wewe ni Mkristo? Samba akajibu, Nyamaza, huko kwenu hamsali kabla ya Kula? Kusikia hivyo Mkulima akaanguka akazimia maana alijua Simba alikuwa anasali kabla ya Kumtafuna!
Mafundisho ya Dini ya Kikristo katika Biblia yanasema; Si kila aniitaye Bwana Bwana ataurithi ufalme wa Mbinguni, ila wale wazitendao kazi za Mungu.
Hivyo usidhani kila wanaopiga magoti wanamwabudu Mungu wa kweli, wengine wanapiga magoti kumbe roho zao ni kama za Simba, wapo kwa ajili ya kukuangamiza kama ilivyo kwa wanasiasa wenye tambo za kuwasaidia watanzania jukwaani kumbe wanakwapua mali ya umma.
Tanzania tuna Kauli Mbiu nyingi za viongozi zisizo na Tija, Mashiko au Utekelezaji. Mfano; Kilimo Kwanza sasa kimekuwa kilimo Mwisho, Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, sasa imekuwa Maisha Mabovu kwa Kila Mtanzania isipokuwa vigogo.
Tuliambiwa hatuwezi kuwaacha Majambazi watambe, lakini siku hizi wananyang’anywa Mali zao Mchana kweupe barabarani, Watu wanamwagiwa tindikali ovyoovyo hadharani, Wandishi, Viongozi wa Dini na wananchi wanauawa na kuteswa tena watanzania wenzi wao.
Sasa naamini mafundisho ya Dini yanayosema, Adui wa Mtu ni watu wa nyumbani Mwake, hivyo yawezekana baadhi ya Viongozi wetu wa Chama na Serikali wasio na Utu na hofu ya Mungu Wakawa kama Simba wamepiga Magoti kwa maana ya kusali kumbe wanatuangamiza.
Lakini yawezekana baadhi ya Viongozi wako kama Mkulima wanaoamua kutekeleza amri kama alivyo Jeshini Ndiyo Afande bila kuhoji, ambapo wakiambiwa kitu wanaingia kwenye utekelezaji kwa mazoea bila kujua madhara yake kwa lengo la kumfurahisha Afande hata kama kuna shida.  Ilimradi bora liende.
Hivi karibuni, tumesikia na kuona uzinduzi wa Mbwembewe wa Kauli Mbiu ya Matokeo Makubwa sasa (Big Result Now) kwa wizara Sita hapa nchini. Kauli hiyo imeanza na vituko kwa upande wa Walimu kwa Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi, huku katika Semina zao.
Ni matokeo makubwa gani sasa, ambayo washiriki kwenye Semina wanakosa Posho na hata kulala kwenye Vitanda wawili wawili?. Mkoani Dodoma katika Sekondari ya Dodoma ilifikia walimu wakafanya Mgomo; kwa nini tunapenda kukurupuka?
Mapema tulimsikia Waziri Dk. Harrison Mwakyembe kwenye Jukwaa la Kisiasa, akijinasifu kuwataja Majina ya Vigogo na Waasisi wa Madawa ya kulevya. Pamoja na kujtutumua kwa wafanyakazi wa Bandari na TAZARA kwa kipindi fulani, tulishuhudia wafanyakazi TAZARA wakifukuzwa kazi ingawa wao ndio walionyimwa Mishahara yao miezi 4.
Tabia hiyo ndiyo ninayosema ni ya Simba kupiga magoti akijifanya anaomba mbele ya Mkristo, ambayo nia yake ni kumtafuna! Hata hivyo kuwaacha Viongozi wa TAZARA wajigambe kuwafukuza wafanyakazi wakati wao ndio wenye kosa la  kutowalipa mishahara, ni sawa na Simba kumwambia Mkristo huko kwenu watu hawaombi kabla ya kula?
Kauli nyingine ya kisiasa nisiyoipenda Jukwani ni ile ya Waziri wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli, ambayo hivi karibuni mkoani Iringa aliridhia kumuongezea Mkataba wa Kichina wa Ujenzi wa barabara ya Dodoma - Iringa, ambapo awali alikataa na kuapa karibu ameze moto.
Aidha binafsi sipingi kuongezewa Muda ili tukamilishiwe barabara, lakini najiuliza Magufuli ninayemfahamu mimi, amelambishwa asali gani, au amepozwa kiasi gani hata abadili kauli yake? Siamini Magufuli kama anaweza kula matapishi yake! Lakini ndiyo hivyo tena karidhia!.

No comments:

Post a Comment

Pages