December 25, 2013

ASKOFU MALASUSA AKEMEA RUSHWA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk. Alex Malasusa akimpa mkono mmoja wa watoto waliohudhuria ibada ya Krismasi katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Francis Dande)
Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki wakiwa katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi katika kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.


 Watoto wakisoma biblia wakati wa ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front.
 Kwaya Kuu ikiimba nyimbo za kumsifu Mungu, wakati wa ibada ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa la Azania Front Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk. Alex Malasusa  akimbariki mtotoTikisaeli Shoo mara baada ya ibada ya Krismasi kumalizika kanisani hapo. 

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front, Alex Malasusa, amewataka viongozi kuacha tabia ya ubinafsi na rushwa kwa kujilimbikizia mali huku waliowengi wakiishi katika lindi umasikini.

Kauli hiyo aliitoa, wakati alipokuwa akizungumza na waamini kwenye ibada  ya kusherehekea kuzaliwa Yesu Kristo, iliyofanyika leo kwenye Kanisa hilo jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana, ubinafsi, rushwa  na tawala za kijanja, janja kama zile za enzi ya Herodi, zimefanya dunia kutawaliwa, maovu kila kona pamoja kulipizana visasi.

“Dunia hii leo imejaa maovu kila kona, watu wanatumia hela nyingi kwa ajili ya kujipatia silaha za kivita hali hiyo inatokana na watu kutotaka kuishi kwa amani”alisema Askofu Malasusa.

Askofu Malasusa, alisema kuna watu wako tayari kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua silaha za kulinda madaraka na kulipiza kisasi.

“Huu ni wakati wa jamii kuwaepuka baadhi ya watu ambao hawapendi kuwaona watu wakiishi kwa mshikamano na amani”alisema Askofu Malasusa.

Aliongeza kuwa wataka viongozi hao wakisherehekea siku kuu hiyo, ni lazima watumie nyadhifa zao za kiserikali kutenda haki na kusimamia maendeleo ya kiuchumi katika jamii.

Aidha, amewakemea baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitoa mafundisho mabaya kwa watu ili waitumie vibaya dini, hivyo ni lazima waamini waishike imani yao na wasikubali kupotoshwa.

Naye Askofu Msaidizi Mkuu wa Jimbo Kuu la Wakatoliki, Dar es Salaam, Dk Eusebius Nzigilwa, alishangazwa na tabia ya baadhi ya watu pindi wapatapo uongozi kushindwa kupigania haki na baadala yake wanajikusanyia mali huku wakiwaacha waliowengi wakitaabika kwa masikini.

“Hata hapa wapo viongozi hao wanaopenda kujilimbikizia mali kwa ajili ya maslahi binafsi pamoja na rafiki zao”alisema Dk Nzigilwa.

Dk Nzigilwa alisema wanataka kuwaona watu ambao wako tayari kupoteza nyadhifa zao kwa ajili ya kupigania haki ya waliowengi

“Na ndio vyo viongozi wetu wanatakiwa kufanya, kwa kuzitumia nafasi zenu kutasaidia kuinua maisha katika jamii mfano alivofanya Yesu ”.

Aidha, aliwataka watanzania kudumisha amani na mshikamano hasa wakati wa hatua hii ya nchi kuelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Dk Nzigilwa alisema anatarajia mambo yatakayoingizwa kwenye katiba hiyo yatakuwa ni yale yatakayoleta haki katika kusimamia rasilimali kwa ajili ya kukuza ustawi wa kila mmoja katika Tifa hili.

No comments:

Post a Comment

Pages