Na Mwandishi Wetu
MANISPAA ya Kinondoni jijini
Dar es Salaam imejikuta ikiwa katika wakati mgumu, kutokana na kitendo cha
kuligeuza eneo la barabara kuwa eneo la
wazi na kuiruhusu Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, kuliboresha kwa
ajili ya kulifanya kuwa maegesho ya magari kinyume na taratibu za mipango mji.
Eneo hilo lililopo Tindiga
mtaa wa Mikocheni ‘ A’, kiwanja namba 269, 270, 271 na 272, linadaiwa kuwa ni
sehemu ya barabara ambayo inaanzia nyuma ya Shule ya Awali ya Feza, inayopita
Nyumbani kwa Rais Ally Hassan Mwinyi na kutokezea Kawe.
Kwa mujibu wa barua
iliyoandikwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ya Machi 8, 2013
na kusainiwa na Mhandisi wa Manispaa hiyo Injinia Uriyo G. A, imeonyesha kwamba
mwekezaji ameruhusiwa kuboresha eneo lililo nyuma ya Kiwanja namba 270, kama
eneo la wazi.
Barua hiyo inaeleza kuwa eneo
hilo ni la wazi, hivyo linabaki kuwa mali ya Manispaa na kwamba
litakapohitajika kwa matumizi ya umma, litatakiwa kuachiwa bila ya pingamizi.
Hata hivyo, barua hiyo
inafafanua kuwa gharama za kuboresha eneo hilo kwa mujibu ramani
iliyowasilishwa na mwekezaji huyo zitakuwa juu yake na haruhusiwi kujenga
‘structure’ yoyote ndani ya eneo hilo la wazi.
“Kabla ya kazi kuanza na wakati
kazi ikiendelea mwekezaji anatakiwa kuwasiliana na ofisi ya Mhandisi wa
Manispaa kwa ukaguzi na ushauri,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, imeelezwa kuwa kwa
mujibu wa uchunguzi wa awali, mwekezaji huyo, amejenga ukuta ambao umeziba
barabara hiyo kuanzia upande wa kutokea shule ya Feza, kiwanja namba 269 na
upande wa pili wa kuelekea kwa Rais mstaafu Mwinyi Kiwanja namba 272 kinyume na
maombi yake ya kuboresha eneo la wazi lililo nyuma ya kiwanja namba 270.
Barua ya maombi iliyosainiwa
na Ephraem Mrema kwa niaba ya Trans Auto
Express Ltd, inaonyesha kwamba Kampuni hiyo ni ya wazalendo na inamiliki
kiwanja namba 270 Keko Avenue, Mikocheni ambapo hapo awali waliipangisha nyumba
hiyo kwa shirika la Kimataifa la Misaada Oxfam na baadaye Taasisi ya Moyo
(Tanzania Heart Institute).
Barua hiyo inaendelea kusema
kwamba nyuma ya eneo hilo upande wa mashariki kuna eneo la Tindiga ambalo kwa
muda wote limetelekezwa siyo tu na wote walio na viwanja vinavyopakana na eneo
hilo bali pia na Manispaa ya Kinondoni.
Hata hivyo, barua inaonyesha
kuwa Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, imeiomba Manispaa kibali cha
kuliboresha eneo hilo la wazi kwa kulisafisha, kuchimba na kutupilia mbali
udongo wa juu kwa kina cha mita moja, kuweka mawe na tabaka gumu (base course),
kusindika na kuweka paving blocks pamoja na mifereji ili kutoa maji na
kuyapeleka kwenye mkondo wake wa asili.
Kwa mujibu wa barua hiyo eneo
linaloombwa lina ukubwa wa takribani mita za mraba 2,300, wamekadiria kuwa
litawagharimu kiasi cha shilingi milioni 200 kwa kazi za awali na shilingi
milioni 12 kila mwaka kwa ajili ya kulitunza.
Hata hivyo, vyanzo vyetu
vimebaini kwamba kuna makubaliano mengine ya malipo ya kila mwenzi kwa
mwekezaji kuilipa Manispaa shilingi milioni 1,960,000 kama kodi ambayo haijabainishwa
katika barua ya Manispaa kumjulisha
mwekezaji.
Baadhi ya majirani wa eneo
hilo wanahoji ni kwa vipi mwekezaji huyu atumie zaidi ya milioni 200 kwa ajili
ya kuliboresha eneo hilo tu na shilingi milioni 12 kila mwaka kulitunza na
milioni 1, 960,000 kila mwenzi kama kodi.
Majirani hao wanahoji, iweje
Manispaa iruhusu Kampuni mmoja kulipatia eneo hilo kwa ajili ya kuliboresha,
wakati kama ingetoa ruhusa ya kila mwenye nyumba afanye maboresho ingewezekana
na wangeweza kuilipa Manispaa shilingi 100,000
kwa kila Nyumba kwa mwenzi na wangeweza kusanya shilingi 400,000 kwa mwenzi, tofauti na mwekezaji huyo
anayelipa shilingi 163,000 kwa mwenzi.
Vyanzo vyetu, vimebaini
kwamba hakuna makubaliano ya mkataba ulioingiwa baina ya Manispaa ya Kinondoni
na mwekezaji Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, juu ya masharti waliyopeana, na
wala hakuna majibu ya barua ya Machi 8, 2013 ya kukubali masharti
waliyokubaliana.
Inasemeka kwamba mradi huo
umewashirikisha mmoja wa kigogo wa cheo cha juu wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA
na mwinge wa ngazi ya juu wa serikali, jambo ambalo limepelekea Manispaa
kukubali kwa urahisi sana kulitoa eneo hilo la barabara na kuligeuza eneo la
wazi na kuiruhusu Kampuni hiyo kuliboresha kwa ajili ya matumizi yake
wanayotalajia.
Kampuni hiyo Trans Auto
Express Ltd ina husika na kupakua na kupakia mizigo inayoingia na kutoka nje ya
nchi (clearing na forwarding).
Uchunguzi wetu, umegundua
kuwa eneo hiyo linataka kugeuzwa kuwa sehemu ya kuhifadhia makontena na magari
madogo yatakayoingizwa nchini na mingine ya nchi za jirani yanayotolewa
bandarini ambayo yatahifadhiwa mahali hapo.
Alipotafutwa Ephraem Mrema ili
kutoa ufafanuzi kuhusu barua ya maombi kwa niaba ya Kampuni ya Trans Auto
Express Ltd, alisema kuwa hausiki na
kitu chochote kwa maelezo zaidi afutwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.
“Mimi sihusiki na kitu
chochote nimeshamalizana na watu wa Manispaa na wala mimi siyo Mkurugenzi wa
Kampuni hiyo ni mwajiliwa tu kama anavyo ajiliwa mtu yeyote yule” alimaliza
kusema Mrema.
Mwandishi wetu alipowasiliana
na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mussa Natty, amewataka viongozi wa
serikali ya Mtaa wa Mikocheni, wilaya ya Kinondoni kusimamia sheria za ujenzi
katika maeneo mbalimbali ili kuepuka migogoro kati ya wananchi na serikali.
Natty alisema kuwa watendaji
hao hawapaswi kukaa kimya pindi
wanapobaini mwekezaji akijenga katika maeneo ya wazi ama ya barabara kwa
matumizi yake binafsi, kwa kuwa sheria zipo wazi na kila mmoja anapaswa kuzitii
bila shuruti.
Mkurugenzi huyo aliendelea
kusema kuwa iwapo kuna yeyote aliyejenga katika eneo la wazi na kusababisha
adha kwa wengine, ni muhimu watendaji wakachukua hatua kutokana na mwekezaji
huyo kuvunja sheria.
No comments:
Post a Comment