December 23, 2013

MSAMA AMWAGA MISAADA YA MIL 5/-KWA YATIMA DAR
Msama akisaidia kushusha vitu katika gari.
Picha ya pamoja.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Krismasi, Alex Msama akimkabidhi sehemu ya msaada wa vyakula mlezi wa kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Mwandaliwa kilichopo Mbweni jijini Dar es Salaam, Halima Mpeta. 
Mlezi wa Kituo cha Yatima cha Malaika Kids, Mwanaid Ramadhani akipokea zawadi za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kutoka kwa Msama.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Krismasi, Alex Msama akimkabidhi zawadi za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, mlezi wa kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Yatima Group cha Mbagala Chamanzi jijini Dar es Salaam, Haruna Mtandika. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Jumla ya vituo vitano vilinufaika na msaada wa sukari, unga, mafuta, sabuni pamoja na mchele. (Picha na Francis Dande)

Na Francis Dande

KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha la muziki wa injili la Krismasi litakalozinduliwa kesho Uwanja wa Taifa chini ya uratibu wa kampuni ya Msama Promotions, jana walitoa msaada wa vitu mbalimbali kwa vituo vitano vya yatima vya jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi msaada wa vitu hivyo vyenye thamani ya shilingi mil 5, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya maandalizi, Alex Msama ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, alisema fedha hizo zimetoka kwenye mfuko wa Tamasha hilo linalofanyika mara ya kwanza.

“Tumeamua kutoa msaada huu kwa yatima kutokana na kuguswa na hali yao hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikuu ya Krismasi, tumeamua kutoa hiki kidogo ili nao wajisikie furaha kama watoto wengine wenye wazazi wao,” alisema Msama.

Msama alisema japo ni mara ya kwanza kufanyika kwa Tamasha hilo la Krismasi tofauti na lile la Pasaka ambalo liliasisiwa mwaka 2000, bado wakaona watoe kiasi kidogo wakiamini watoto watafarijika  katika sikukuu hiyo.

Vituo vilivyopata misaada hiyo ya kiutu ambayo ni pamoja na Mwandaliwa cha Mbweni, Mahabusi ya Watoto jijini Dar es Salaam, Yatima Group cha Mbagala, Malaika Kidds cha Mwananyamala na kingine ambavyo jumla yake ni vitano.

Akipokea msaada huo jana katika Ofisi za Dira Mtanzania Publishers Ltd, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Ofisa Mfawidhi wa Mahabusi ya Watoto, Ramadhani Yahya, alishukuru na kuwataka wengine waige mfano wa Msama kuyakumbuka makundi maalumu katika jamii.

Naye Halima Mpeta wa Kituo cha Mwandaliwa cha Mbweni, alisema anashukuru kwani msaada huo sio tu umekuwa faraja kwa kituo hicho na watoto, pia umekuja wakati muafaka kuelekea Krismasi ambapo ni faraja kubwa kwa watoto hao wenye mahitaji.

Msama amekabidhi misaada hiyo ikiwa ni siku mbili kabla ya uzinduzi wa Tamasha la Krismasi litakalofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa ambapo waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania,  watahudumu.

Waimbaji wa Tanzania, ni Rose Muhando, Upendo Mkone, Upendo Kilahilo, Edson Mwasabwite, John Lissu na New Life Band. 

Kutoka nje ni Solly Mahlangu kutoka Afrika Kusini, Solomon Mukubwa (Kenya), Liliane Kabaganza na Ephraim Sekeleti kutoka Zambia ambao walishaanza kutua nchini tangu juzi.

Msama alisema, mbali ya malengo ya msingi ya tamasha hilo ambayo ni kueneza injili kwa mataifa yote kupitia vipaji vya uimbaji, sehemu ya mapato yataelekezwa katika ujenzi wa kituo cha yatima kitakachojengwa eneo la Pugu, jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Pages