Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye (pichani), amesema vijana wakiwezeshwa kikalimifu kushiriki shughuli za uzalishaji, umasikini Tanzania utakuwa historia.
Pia, amewaasa vijana kutumia elimu walizonazo katika kujiajiri ili kuharakisha maendeleo badala ya kukaa vijiweni na kubaki kuwa walalamishi na wakati mwingine kutumiwa na wanasiasa kama ngazi ya kutimiza malengo yao.
Kangoye, ambaye amekuwa mhamasisha mkubwa wa vijana nchini, amesema Tanzania inaweza kuwa taifa linalotoa misaada kwa nchi zingine na kuachana na utegemezi iwapo vijana wataitambua na kutumika kikamilifu kwa shughuli za maendeleo.
Aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na vijana katika sherehe za kusimikwa Kamanda wa UVCCM wilaya na makamanda wa Kata wilayani Kongwa, ambapo Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, alisimikwa kuwa Kamanda wa Vijana wilaya.
Kangoye, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliema Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Nelson Mandela ni alama ya harakati za vijana katika maendeleo na ukombozi wa Bara la Afrika na kwamba, walianzisha mageuzi hayo wakiwa vijana.
‘Vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kukataa umasikini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mageuzi ya kiuchumi katikka taifa letu. Tanzania inaweza kuwa taifa linalotoa misaada badala ya kuwa tegemezi iwapo vijana watajitambua na kuitoa kuleta maendeleo.
‘Muda wa kukaa vijiweni na kuilalamikia serikali haupo, tuna fursa na rasilimali nyingi zinazoweza kuleta mageuzi ya kiuchumi na kutufanya kuwa taifa tajiri,’ alisema Kangoye.
Alisema harakati zozote ziwe na kisiasa, kiuchumi na kijamii huanzia kwwa vijana na kwamba, ni wakati sasa wa kuamka na kuleta mageuzi kwa maslahi na ustawi wa Tanzania ya sasa na inayokuja.
Naye Ndugai akizungumza baada ya kusimikwwa kuwa Kamanda wa Vijana wilayani humo, aliungana na Kangoye kwa kuwataka vijana kujituma katika shughuli za uzalishaji ili kuacha kuwa tegemezi.
Alisema kuna vijana wengi wenye elimu na ujuzi wa kutosha, lakini hawataki kufanya kazi na badala yake wanasubiri serikali iwafanyie kila kitu, jambo ambalo amesema haliwezekani.
‘Tufanye kazi ndugu zangu ili tuachane na umasikini na kuwa tegemezi, fursa zipo za kutosha kinachotakiwa ni kuamua kama alivyosema DC Kangoye ili tulete mageuzi kwenye taifa letu’ alisema.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kongwa, Asia Alamga, alisema kabla ya kuwasimika makamanda hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kutembelea wafungwa, wagonjwa kwenye hospitali za wilaya na kata na kutoa misaada ya kijamii.
No comments:
Post a Comment