January 23, 2014

OKWI APIGWA STOP KUICHEZEA YANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo (Januari 22 mwaka huu) kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.

Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

Katika FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Hivyo, TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.

MECHI ZA TANZANIA PRISONS YAZASOGEZWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesogeza mbele mechi za raundi ya 14 na 15 zinazoihusu timu ya Tanzania Prisons zilizokuwa zichezwe Januari 25 na 29 mwaka huu.

Awali Tanzania Prisons ilitakiwa kutafuta uwanja mwingine wa kuchezea mechi hizo dhidi ya Ruvu Shooting na JKT Ruvu kutokana na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine kutokuwa tayari kwa Ligi Kuu ya Vodacom wikiendi hii.

Mechi hizo sasa zitachezwa kati ya Februari 6 na 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages