February 13, 2014

Extra Bongo yanyakuwa wawili Twanga Pepeta
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa wakali wa muziki wa dansi nchini Extra Bongo ‘Next Level Wazee wa Kimbembe’ umemrejesha kundini aliyewahi kuwa rapa bendi hiyo Greyson Semsekwa sambammba na kumnyakuwa mnenguaji Asha Sharapova kutoka bendi ya African Stars Twanga Pepeta.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa bendi hiyo Juma Kasesa, alisema, kurejea kwa Semsekwa mmoja ya wanamuziki waasisi wa Extra Bongo kutaimarisha safu ya 'kufokafoka' kuelekea kwenye uzinduzi wa albamu yao mpya ya 'Mtenda Akitendewa.'

Kwa mujibu wa Kasesa, Mtenda Akitendewa inatarajiwa kuzinduliwa Februari 22 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live, uliopo Mbagala Zakhiem  jijini Dares Salaam.

Semsekwa alishiriki kwa kiwango katika albamu ya 'Mjini Mipango' mwaka 2009 kabla ya baadae kutimkia Twanga Pepeta na sasa amerejea kundini akiwa na rapu mpya ambazo atazimbulisha Jumamosi hii katika onyesho maalumu la Utambulisho wao litakalofanyika katika Ukumbi wa Meeda Sinza.

Alisema, wameamua kumchukua Sharapova baada ya kutambua kipaji alichonacho katika unenguaji hivyo kukidhi vigezo vya kunengua kwenye bendi hiyo inayoundwa na wanenguaji wakongwe kama Maria Salome na Otilia Boniface chini ya ukufunzi wa Super Nyamwela.

"Tunaendelea na mikakati ya kujiimarisha kwakuwa kila maboresho tunayofanya kwenye bendi pia tunazingatia maoni na ushauri wa wapenzi na wadau wa Extra Bongo ili kuendelea kuwapa burudani inayowasuuza nyoyo zao,"alisema Kasesa.


Aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi hii kwenye onyesho la bendi hiyo Meeda kuona muonekano mpya wa Semsekwa na Sharapova baada ya kutoka Twanga Pepeta.

No comments:

Post a Comment

Pages