MATUKIO ya utelekezaji wa mke na watoto nchini Tanzania bado ni changamoto kubwa katika jamii. Licha ya matukio haya kutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine bado yanachochewa na kulegalega kwa sheria za nchi ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa baadhi ya vipengele.
Waathirika wakubwa wa matukio haya ni mama pamoja na watoto ambao ndio hutelekezwa huku baba aliyetelekeza familia hiyo kutokomea sehemu nyingine na kwenda kuanzisha familia nyingine, ambayo nayo uhai wake huwa mashakani.
Hivi karibuni mwandishi wa makala haya kwa ushirikiano wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA); alifanikiwa kutembelea Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa na kufanya utafiti wa kihabari kuangalia matukio ya kiunyanyasaji na ukatili ambayo huwakumba wanawake na watoto katika wilaya iliyotajwa.
Maria Tarafa (25) mkazi wa Kijiji cha Isale, Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa akinamama ambao amekumbana na matukio ya utelekezwaji. Mama huyu ameachwa kisheria na mumewe akiwa tayari wamefanikiwa kupata watoto wanne bila kufanyika mgawanyo wa mali walizochuma na mumewe.
Hata hivyo huenda tukio la kuachwa kwa Bi. Tarafa lisimuumize roho kama ilivyo tukio la mume aliyemuacha yaani Bw. Ndebile Kazuri (31) kumtia ujauzito akiwa darasa la sita katika Shule ya Msingi Isale mwaka 2004 na kumkatisha masomo yake kabla ya kumuoa. Taarifa zinaonesha binti huyu alipewa ujauzito akiwa na miaka 15 na kujifungua akiwa na miaka 16 na papo hapo kufunga ndoa ya kimila kijijini hapo.
Akizungumzia mkasa mzima, Bi. Tarafa anasema baada ya Kazuri kumkatisha masomo yalifanyika mazungumzo ya kifamilia bila ya yeye kujua na alishangaa kuona mzazi wake (ambaye sasa ni marehemu) amepokea mahari kasha yeye kuozeshwa kimila kwenda kwa mumewe.
Aliishi kwa mume huyo tangu kipindi hicho na kuzaa naye watoto wanne, lakini visa na mateso kwa mwanaume vilianza akiwa na watoto wawili. Anasema mume wake alikuwa akimpiga ndani ya ndoa yao na baada ya kuona mateso yamezidi aliondoka na kurudi nyumbani.
Anasema baada ya tukio hilo mumewe alitafuta wazee wa ukoo na kumfuata tena nyumbani kwao na kumuomba samahani ili wamalize tofauti zao na kurudi kwa mumewe. Anasema baada ya kumuomba aliridhia na kurudi kwa mumewe akiwa na watoto wake wawili.
Bi. Tarafa anasema baada ya kurudi waliongeza idadi ya watoto na kufikia wanne kwa mumewe huyo. Vipigo na manyanyaso viliendelea na safari hii mumewe akitamka wazi wazi kuwa anataka kumuacha hivyo arudi nyumbani kwa wazazi wake tena na watoto wote. Uamuzi huu ndio uliomkera mwanamama huyu na kuamua kudai haki zake za msingi pamoja na watoto wake.
Mumewe ambaye kwa sasa anamke mwingine akiwa anaishi naye, alifungua kesi namba 26/2013 katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28, 2013, akitaka mahakama ivunje ndoa yake na mkewe kwamba amemchoka kutokana na kile kugombana naye mara kwa mara.
Kwa mujibu wa nakala ya huku ambayo mwandishi wa makala haya anayo, kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwenye nakala ya hukumu kwa jina la B. Stanley; ilitolewa hukumu Novemba 18, 2013 na mahakama kuvunja ndoa hiyo.
Mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili (wa chini ya miaka saba) kati ya wanne waliozaa na mumewe bila kueleza namna watoto hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao ambaye tayari anatengana na mumewe.
Mahakama hiyo pia katika hukumu yake iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Kwa mujibu wa nakala ya hukumu mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote msimu wa kilimo ulioisha na bati 7 zilizokuwa nyumbani kwao.
Bi. Tarafa anasema haridhiki na namna ilivyotolewa hukumu ya kuvunja ndoa yao. Anasema kwanza sababu zilizotolewa na mumewe mahakamani hazina ukweli wowote na pia hakupewa nafasi ya kujitetea hadi hukumu ya ndoa yao ikisomwa.
Anasema pamoja na hayo mahakama imevunja ndoa yao, na kwa sasa hawezi kung’ang’ania ndoa hiyo irejee lakini anachokitaka ni haki yake pamoja na watoto ipatikane toka kwa aliyekuwa mumewe. Anasema walichuma mali nyingi wakiwa pamoja lakini mali hiyo haikuzungumziwa kabisa mahakamani.
“…Inaniuma sana kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani alinikatisha masomo, kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa watoto wanne na anataka niende kuishi nao peke yangu nyumbani kwetu,” anasema Bi. Tarafa.
Anasema wakati mumewe anafungua kesi ya kutaka mahakama ivunje ndoa yao aliiongopea mahakama kwamba hawana mali yoyote nyumbani jambo ambalo si kweli. “…Mume wangu alidanganya kuwa hatuna mali pale mahakamani, mimi nikaeleza ni uongo kwani tuna ng’ombe zaidi ya 127, buzi 30, nyumba mbili pale kijijini Isale pamoja na hekari zaidi ya 70 za mashamba…hawakunisikiliza pale mahakamani. Ukweli ni kwamba tunamali hizo ambazo tulichuma tukiwa wote,” anasema Bi. Tarafa.
Akifafanua zaidi anasema walipewa ng’ombe za urithi toka kwa baba yake na Kazuri zikiwa 65 lakini wamezizalisha hadi kufikia idadi zilipo sasa pamoja na mashamba na nyumba lakini anashangaa mzazi mwenzake anamdhulumu kila kitu.
Kimsingi nakala ya hukumu ya kesi iliyovunja ndoa ina kurasa tatu pekee, ambazo mwandishi wa makala haya amezipitia na ukweli ni kwamba hakuna sehemu hata moja imezitaja mali anazozilalamikia Tarafa. Na pia hukumu hiyo haikuonesha namna/utaratibu wa watoto wanaobaki kwa mama watakavyo hudumiwa na baba.
Pamoja na hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Ramadhan Rugemalira anasema mama huyo anahaki ya kufungua kesi ya madai kuomba mgawanyo wa mali na matunzo kwa watoto endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa kwa shauri hilo.
“…Anachotakiwa kuomba mahakamani kwa sasa ni mgawanyo wa mali, kwamba katika kesi yao ambayo mahakama ilivunja kuna mali ambazo mahakama haikuzizungumzia kabisaa lakini na mimi (mke) ninahaki na mali hizo, unaona…ataleta ushahidi kama ng’ombe hao wapo kama kuna ardà na nini…hivyo huyo mwanaume ataitwa na kesi kusikilizwa,” anasema Rugemalira katika ushauri wake akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Anaongeza kuwa, huenda mtoa hukumu wa mwanzo aliteleza kwa kitendo cha kutoainisha namna watoto wanaobaki kwa mama watalelewa vipi. Anasema pamoja na hayo bado mama huyo anahaki ya kufungua madai mengine kudai haki hizo.
Pamoja na hayo, kwa kuzingatia Sheria nyingi kama vile Sheria ya Mtoto (2009), Sheria ya Ndoa (1971), Sheria ya Kanuni za Adhabu (1937) n.k. pamoja na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na kusainiwa na taifa, ni vyema sasa kila mtu, kwa nafasi yake mzazi/mlezi, na hata mamlaka kuwa ustawi na maendeleo ya mtoto ni jambo lamsingi.
Sheria ya Ndoa (1971), kifungu 114 kinaeleza uwezo wa mahakama kutoa amri ya kugawana mali za waliooana na pia kuzingatia masilahi ya watoto na usawa katika ugawaji. Pia kifungu 136 (1) kinaeleza uwezo wa mahakama kuzingatia nasaha za maofisa wa ustawi kiushauri. Sheria ya Mtoto (2009) pia inaeleza maana ya mtoto, lakini pia inatoa agizo la wajibu wa mzazi/mlezi kwa mtoto au watoto.
Kwa upande wake Kazuri akizungumzia mali ambazo mke anazilalamikia, yaani ng’ombe 127, nyumba 2, mbuzi 30 na ardhi hekari 70 anasema mali hizo alipewa na babayake wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake ambaye alidai yupo hai hadi sasa. Uchunguzi uliofanywa umebaini baba yake na Kazuri (yaani Kazuri Moshi) alifariki dunia tangu Machi 2004 na mali zake kugawiwa kwa watoto wake.
Hata hivyo tayari Bi. Tarafa amefungua kesi nyingine mahakama ya mwanzo akiitaka mahakama igawe mali walizochuma na mumewe kipindi chote na kuweka bayana majukumu ya namna watoto wa wanandoa hao waliotengana watapata mahitaji yao kutoka kwa baba yao.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA
No comments:
Post a Comment