October 27, 2014

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA), YAIPIGA JEKI MIILIONI 5 SHULE YA SEKONDARI LILIAN KIBO

 Mgeni rasmi, Mwanasheria Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wakili Msomi, Ramadhan Maleta (katikati mwenye tai) akiangalia kazi za wanafunziza darasani  walizozionesha kwake na kwa wazazi wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya Lilian Kibo, Goba Matosa, Dar es Salaam juzi.
 Wakili Maleta akiangalia chura anavyopasuliwa wakati wa somo la bailojia wakati akioneshwa na mwanafunzi wa shule ya Lilian Kibo.
Wanafunzi wa shule ya Lilian Kibo wakitumbuiza kwa nyimbo wakati wa mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo juzi.
Baadhi ya wazazi wakiserebuka na wanafunzi kusherehekea mahafali.

 XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imetoa wito kwa wanafunzi wote nchini, kusoma masomo yatakayowawezesha kufanya kazi katika sekta ya anga kwani sekta hiyo ina uhaba wa wataalam nchini.

Rais hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa TAA, Wakili Msomi, Ramadhan Maleta wakati akihutubia katika mahafali ya nne ya shule ya sekondari ya Lilian Kibo, Goba Matosa, Dar es Salaam Jumamosi.

Wakili Maleta aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleiman Said Suleiman aliye China kwa ziara ya kikazi na Rais Jakaya Kikwete alisema, ni aibu kwa nchi kuajiri wataalam wa nje katika sekta hiyo kwa sababu tu wanafunzi wameshindwa kuichangamkia.

“Sisi kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege tunategemea sana juhudi zenu kama shule ili tuweze kupata wataalam wakiwemo marubani, wahandisi, waongoza ndege, wanasheria, wahudumu wa kwenye ndege (air hostess). Kutokana na hali hiyo, tutakuwa tayari wakati wowote kushirikiana nanyi kwa hali na mali pale inapobidi kuona kuwa vijana wetu wanaandaliwa kwa kiwango kinachostahili ili tuweze kuwa na wataalam wa uhakika, “ alisema katika hotuba yake.

Mwanasheria huyo aliwaeleza wanafunzi wa Lilian Kibo kuwa, hivi sasa sekta ya usafiri wa anga inalipa na ina nafasi nyingi za ajira kwa wale ambao wana taaluma stahiki akiwataka wasijazane kusoma fani ambazo hivi sasa zina wataalam wengi kiasi cha wengine kukosa kazi.

“Natoa rai kwa vijana mnaomaliza na hata ambao bado mpo katika vidato vya chini, muongeze juhudi katika masomo yenu kwani Taifa na hata sisi tulio katika sekta ya usafiri wa anga tunawategemea muwe wataalam wetu hapo baadaye. Sekta ya usafiri wa anga kwa sasa inakua kwa kasi sana lakini haina wataalam wazalendo wa kutosha kwani vijana wengi hawana msukumo wa kwenda huko,” alisema.

Aliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kazi nzuri ulioifanya ya kuwalea vijana kielimu na kufanikisha kupeleka vijana wote 22 wa kidato cha sita katika vyuo vikuu vya Mzumbe, Sokoine, SAUT, Dar es Salaam, Chuo cha Uhasibu (TIA), IFM baada ya kufaulu kwa daraja la kwanza na la pili tu katika masomo ya sayansi na sanaa mwaka 2013.

Hata hivyo, aliwapa changamoto wanafunzi waliohitimu kidato cha nne kuongeza jitihada zaidi katika masomo kwani tofauti na zamani, elimu ya kidato cha nne siku hizi ni kama hatua ya awali ya kujifunza.

“Ni hatua ambayo wanapaswa kuichukulia kuwa ni changamoto inayowapa msingi wa kusonga mbele zaidi hadi kufikia kidato cha sita na lengo likiwa ni kufikia chuo kikuu katika ngazi ya shahada ya kwanza na ya pili na ikiwezekana ya tatu, “ alisema Wakili Maleta.

Aliwapongeza walimu, wamiliki na uongozi wa shule hiyo kwa kazi nzuri ya kutoa elimu na akawapa pole kwa kufiwa na mmiliki wa shule hiyo, Kibo Shirima Merinyo miezi sita iliyopita akiwataka waendelee na umoja wao kukabili changamoto mbalimbali zinazoikabili shule.

Katika kuisaidia shule hiyo kutatua changamozo zake, alisema TAA itatoa sh. Milioni tano za kuvuta maji ya bomba shuleni hapo lakini akawataka wazazi waanzishe na kuchangia mfuko wa maji shuleni.

Wakili Maleta alisema, TAA imetoa fedha hizo kwa shule ya Kibo iliyo umbali mrefu sana kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwa kutambua kuwa, hata jamii iliyo mbali ni sehemu ya majirani wa TAA kwa sababu inawahitaji katika vita dhidi ya magaidi, wafanya biashara ya madawa ya kulevya na wanaoharibu miundombinu ya viwanja vya ndege. Alisema, kwa kawaida, TAA husaidia zaidi, shule zilizo jirani na viwanja vyake vya ndege nchini.

“Ni matumaini yangu kwamba, wengi wenu mliopo hapa mmeshatumia au mtatumia viwanja vyetu kwa safari za ndani na nje ya nchi. Pia naamini mnafahamu changamoto za kiusalama za viwanja vya ndege na hasa suala la ugaidi, upitishaji wa madawa ya kulevya, nyaraka za Serikali n.k. Hivyo, kwetu sisi, nyote nyie ni majirani na marafiki zetu katika kusaidia ulinzi wa viwanja vyetu. Ni wajibu wetu kushirikiana nanyi katika masuala ya kijamii kama elimu, “ alisema.

TAA inasimamia, kuendeleza na kujenga viwanja 58 vinavyomilikiwa na Serikati Tanzania bara. Wakili Maleta alisema, hivi sasa Mamlaka inaendelea na mchakato wa ujenzi wa viwanja vipya vya Shinyanga, Sumbawanga kwa kiwango cha lami. Tayari imejenga viwanja vya Bukoba, Mwanza, Songwe, Mafia, Kigoma, Tabora kwa lami pia.

Imetolewa na Ofisi ya Sheria na Uhusiano TAA
Oktoba 26, 2014

No comments:

Post a Comment

Pages