October 08, 2014

MBUNGE WA KAWE AENDA SEGEREA

 Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) ambaye pia ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee akitoka katika Chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kulekea katika Gereza la Segerea baada ya kukosa dhama katika kesi inayoamkabili pamoja na wanachama wenzake ya kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.
 Halima Mdee akielekea kupanda gari la Polisi kuelekea Gereza la Segerea huku akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee akipanda gari la Polisi kuelekea Gereza la Segerea, baada kukosa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. 
 Halima akipanda gari la Polisi tayari kwa safari ya kuelekea gereza la Segerea.
 Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa wameimarisha ulinzi nje ya Mahaka ya Hakimu Mkhazi Kisutu wakati wa kesi ya Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema) ikisikilizwa mahakamani hapo.
Mbunge wa Kawe Halima Mdee (katikati) akiwa na watuhumiwa wenzake muda mfupi kabla ya kuelekea Gereza la segerea.
 FFU  wakiwa wameimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Kisutu.
 Askari wa FFU akiwa nje ya Mahakama kuhakikisha usalama unakuweo wakati wa kesi ya mbunge wa Kawe ikiendelea. 
 Safari ya Segerea inaanza.
 Magari yakitoka Mahakamani.

 Baadhi ya wanachama na wafuasi wa Chadema waliofika Mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo wakipaza sauti zao.



DAR ES SALAAM, Tanzania


MBUNGE wa jimbo la Kawe, Halima Mdee (35), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na wenzake nane, wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.


Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha), alifikishwa mahakamani hapo na wenzake na kusomewa mashitaka na jopo la Mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Bernad Kongola, Salum Mohamed na Hellen Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda.

Mawakili hao waliwataja washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Rose Moshi (45) mkazi wa Kinondoni (b), Renina Peter maarufu kama (Lufyagila) mkazi wa kinondoni mkwajuni.

Wengine ni Anna Linjewile (48), mkazi wa Mbezi Luis, Mwanne Kassim (32), mkazi wa Pugu Kajiungeni, Sophia Fanuel (28) mkazi wa Mbezi Beach, Edward Julius (25) mkazi wa Msasani, Martha Mtiko(27) mkazi wa Mikocheni na Beauty Mmari (35) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni.

Akiwasomea shitaka la kwanza, Wakili Kongola alidai kuwa Mdee na washitakiwa wenzake, mnamo Oktoba 4, 2014, mtaa wa Ufipa, wilaya ya Kinondoni  jijini Dar es Salaam, bila ya kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mratibu wa Polisi(SP), Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi hilo.

Kongola alidai kuwa washitakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 124 cha sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Wakisomewa shitaka la pili na wakili Mohamed, siku hiyo ya tukio katika eneo hilo, washitakiwa hao kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio wa halali kwa lengo moja la kwenda kwenye Ofis ya Rais.

Wakili huyo alidai kuwa, kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 74 na 75 cha Sheria ya Kanuni na Adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika, hivyo waliiomba mahakama kupanga tarehe ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali (PH).

Kaluyenda alidai , dhamana ya washitakiwa hao ipo wazi ambapo kila mmoja  alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za ofisi wanazofanyia kazi pamoja na kitambulisho , huku wakitakiwa kutoa bondi ya sh. milioni moja kwa kila mshitakiwa.
Washitakiwa hao walirejeshwa rumande baada ya wakili kushindwa kumaliza kuhakiki fomu za dhamana zao.  

Aidha, washitakiwa hao waliondolewa kwenye ardhi ya Mahakama ya Kisutu wakiwa chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya polisi 30 na msafara wa magari manne likiwemo la maji ya kuwasha.

No comments:

Post a Comment

Pages