MFANYABIASHARA
wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye kambi za watalii
katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo katika mikoa ya
Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani akiwa
katika baa maarufu ya Arusha Raha iliyopo la Shams, jijini hapa.
Kisa cha
kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya kuligonga gari jingine
katika eneo la Mbauda wakati akitokea katika makazi yake yaliyopo eneo la Kwa
Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa
na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa
maarufu ya Arusha Raha.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo baada ya
kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa wamemzingira
katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari lake aina ya Nissan Navara.
“Alipiga
risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguza wakanywea, akatumia mwanya huo
kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la kujificha,
na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa
inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa haraka
pombe mbili kali aina ya Valuer na wakati anamalizia ya tatu, akajikuta
anazingirwa tena na wale waendesha bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na
kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili nyingine hewani, lakini bila
ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo akaamua kujimiminia risasi.
Habari zaidi
zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi wasamaria wema wakiwa
harakati za kupiga simu polisi walishitukia polisi wakiingia katika eneo la
tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia risasi
kifuani.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio
hilo, ingawa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha imekiri kuwepo kwa
tukio, lakini chanzo chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji
wa matukio ya jeshi hilo mkoani Arusha.
Mwili wa
marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa
Arusha ya Mount Meru.
No comments:
Post a Comment