October 02, 2014

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO MKUU WA KWANZA UMOJA WA VYUO VYA USAFIRI WA ANGA BARANI AFRIKA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi , Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Mbwana . J. Mbwana akisalimiana na Rais wa  Umoja wa Vyuo vya Usafiri wa Anga Barani Afrika(AATO) Tchagbele Sadamba  wakati wa  mkutano mkuu wa kwanza wa AATO  unaofanyika Zanzibar kwa ajili ya kujadili mbinu za kuboresha  mafunzo ya usafiri wa anga barani Afrika. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) Dkt.  James Diu. (Na Mpiga Picha Wetu)

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
 
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano  mkuu wa kwanza wa Umoja wa Vyuo vya Mafunzo ya Usafiri wa Anga Barani Afrika (AATO)  utakaofanyika Zanzibar.

Mkutano huo  wa siku tatu, kuanzia Oktoba 1-3, utakutanisha vyuo vya mafunzo ya usafiri wa anga, wataalamu wa sekta na taasisi nyingine zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga. Kauli mbiu ya Mkutano ni “Uhuishwaji na Viwango vya Mafunzo ya Usafiri wa Anga kwa Usalama wa Usafiri wa Anga Barani Afrika na Kwingineko”.

Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe atafungua mkutano huo wakati, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Juma Duni  Haji atakuwa mgeni rasmi wakati wa kufungwa kwa mkutano.

Wakati wa mkutano huo wajumbe watajadiliana kuhusu ushirikiano wa vyuo vya usafiri wa anga, hatua zilizofikiwa katika kuanzisha vituo vya mfano(center of excellence) vya mafunzo ya usafiri wa anga na uhaba wa wataalam wa usafiri wa anga barani Afrika, changamoto zinazotokana na taaluma mpya za usafiri wa anga na mstakabali wa AATO.

Wajumbe hao pia watapata fursa ya kutembelea  maeneo ya utalii huko Zanzibar. Maeneo hayo ni pamoja na mashamba ya viungo, kisiwa cha Prison maarufu kwa  kobe wakubwa na eneo la mji mkongwe wa Zanzibar.

AATO ilizinduliwa mwaka 2013 huko Abuja, Nigeria kufuatia mapendekezo ya mkutano maalumu wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO AFI- RAN) mwaka 2008 nchini Afrika Kusini. Mapendekezo yalizitaka taasisi za mafunzo ya usafiri wa anga kuwa na mikutano ya pamoja kwa lengo la kuboresha ushirikiano, viwango, ubora  na kuhuisha mafunzo ya usafiri wa anga barani Afrika.

Malengo mkakati ya AATO ni pamoja na kuwa na sauti  ya pamoja ya vyuo  wanachama na  kuhimiza vyuo hivyo kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Vyuo wanachama wa AATO vinapata manufaa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa kwenye ushirikiano na vyuo wanachama, fursa ya kujitangaza na kutambulika zaidi, kuwa na mitaala inayokidhi viwango. Faida nyingine ni kupata  taarifa sahihi kuhusu sekta ya usafiri wa anga

Chuo cha usafiri wa Anga Tanzania(CATC) ni miongoni mwa  wanachama waanzilishi wa AATO pia ni mwanachama wa baraza la AATO ikiwakilisha nchi za Afrika Mashariki. AATO ina vyuo wanachama 30.


 Margareth Kyarwenda
KNY
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA(TCAA).

No comments:

Post a Comment

Pages