November 16, 2014

MAHAKAMA YA KISUTU YAIPIGA TENA TAREHE KESI YA MACHA

Mahakama Kisutu yahairisha tena
kesi ya Macha hadi Nov 18

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi juu ya mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Hans Aingaya Macha (pichani), kama ana kesi ya kujibu au la.

Hali hiyo ilitokana na Hakimu Mkazi wa Kisutu, Devotha Kisoka anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo na Hakimu Janeth Kalkuyenda kusema uamuzi utatolewa Novemba 18.

"Leo kesi ilikuja kwa ajili ya uamuzi, sintoweza kutoa uamuzi hapa, Hakimu mwenye kesi hayupo na uamuzi utatolewa Novemba 18, hivyo naiharisha kesi hadi siku hiyo,''alisema Hakimu huyo.

Macha anashitakiwa kwa kosa kughushi hati ya kiwanja chenye namba 183 kilichopo Kigogo, mali ya Ramadhan Balenga, baada ya kugushi mkataba wa mauziano na hati ya uhamishaji miliki.

Kabla ya mahakama kushindwa kutoa uamuzi huo, Wiki iliopia Hakimu Devotha alisikiliza ushahidi wa mwisho kutoka kwa upande wa mashitaka, ambaye alikuwa Mkuu wa Maabara ya Uchunguzi wa Hati wa Polisi, Mrakibu wa Polisi, Amaan Renatus Saad.

Renatus alidai mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Devotha kuwa alipokea nyaraka kutoka kwa Ofisi ya Msajili wa Hati ikiomba ifanyiwe uchunguzi katika nyaraka za uhamishaji miliki kutoka kwa Balenga kwenda kwa Macha.

"Nina uzoefu wa miaka zaidi 10, ambapo nimeupata sehemu mbalimbali ikiwemo Bostwana. Polisi ilipokea barua kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutaka kufanyiwa uchunguzi,''alidai.

Renatus alidai baada ya kupokea barua, walifanya uchunguzi na kutoa taarifa kwa Wizara ya Ardhi kuwa saini walizochunguza hazikusaini na mtu mmoja, ambaye ni Balenga, hivyo zimegushiwa.

Alidai uchunguzi wao, ulizingatia mambo mengi ikiwemo mgandamizo wa peni, spidi ya peni, hivyo aliiomba mahakama ipokee ushahidi wake kama kielelezo sahihi katika kesi hiyo.

Kutokana na ushahidi huo, upande wa mashitaka unaoongozwa na Wakili wa serikali, Nassoro Katuga, alidai mahakamani hapo kuwa, wamefunga ushahidi na kutoa nafasi ya upande wa utetezi nao kutoa ushahidi wake.

Hakimu Devotha, aliiaharisha kesi hiyo hadi jumatatu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la. kesi anayoshitakiwa Macha ni kugushi mkataba wa mauziano, hati ya miliki na kuwasilisha hati iliyogushiwa kwa Msajili wa Hati.

No comments:

Post a Comment

Pages