HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2014

KIWANDA CHA SUKARI KAGERA CHAZALISHA ZAIDI

Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakioneshwa mashine ya kumwagilia maji miwa ijulikanayo kwa kitaalamu kama Centre Pivot System.
Na Saidi Mkabakuli, Kagera

Kiwanja cha Sukari cha Kagera kimeanza kuzalisha ziada ya sukari inayohitajika katika soko la sukari nchini hali inayopelekea kuweza kupunguza tatizo la upatikanaji wa sukari Tanzania na nchi za jirani zinazotumia sukari kutoka kiwandani hapo.

Hayo yamewekwa wazi na Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Bw. Ashwin Rana, wakati alipokuwa akizungumza na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.

“Kwa sasa tumeweza kuongeza mauzo katika kanda kufikia tani 40,000, pamoja na kuongeza ununuzi kutoka kwa wakulima wa miwa wa nje zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka,” alisema.

Bw. Rana  aliongeza kuwa Kiwanda chake kimewekeza zaidi katika upanuzi wa eneo la shamba la miwa la umwagiliaji la hekta 3600 pamoja na kuwekeza zaidi katika teknolojia ya kisasa katika kilimo.

“Kampuni yetu imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na vifaa vya kisasa ikiwemo matrekta yanayotumia setalaiti katika ufanyaji kazi wake katika kuandaa mashamba,” aliongeza.

Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amekipongeza Kiwanda hicho kwa  kuwekeza kwenye uzalishaji wa kisasa wa miwa hali inayoongeza uzalishaji wa sukari kuwa mkubwa kiwandani hapo.

Bibi Mwanri ameongeza kuwa Kiwanda hicho kinastahili pongezi za kipekee kwa kuweza kuongeza ajira zaidi ya watu 6000 waliopo kiwandani.

“Kwa kweli munastahili sifa kwa kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania pamoja na kuuza umeme kwenye gridi ya Taifa,” alisema.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanda hicho, kwa sasa kinakabiliwa na na changamoto za uuzaji haramu wa sukari zinazoingia kimagendo nchini ambao umechangiwa kushindwa kwa kiwanda kuuza sukari ili kurudisha gharama za uzalishaji kutokana bei za sukari zinazoagiwa kutoka nje kuwa bei ya chini sana.

“Bei ya Sukari Duniani imeshuka sana kutokana na Nchi kubwa duniani kusaidia wakulima katika uzalishaji na pembejeo (subsidies) na hivyo sukari kuuzwa katika soko la dunia kwa bei ya chini (Dumping) na kufanya kuwa bei kuwa ndogo kuliko gharama halisi ya uzalishaji,” aliongeza.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni pamoja na kiwanda kushindwa kulipa mikopo iliyochokuwa benki kutokana na kuwepo sokoni kwa sukari ambayo ni ya magendo na bei ya chini hivyo kiwanda kushindwa kufikia malengo hata ya kiundeshaji na mipango mikakati.

Kiwanda cha Sukari cha Kagera kiko katika sehemu Kaskazini Magharibi ya Tanzania (karibu na mpaka wa Tanzania na Uganda) kilibinafsishwa na Serikali kwa sekta binafsi mwaka 2001.
 Malengo ya ubinafsishaji yalikuwa kuboresha upanuzi wa masoko ya ndani na kikanda, uwekezaji wa kisasa, upanuzi na ukarabati na majengo ili kuhakikisha shughuli za kiundeshaji zinaboreshwa.

No comments:

Post a Comment

Pages