February 06, 2015

TAARIFA KWA UMMA MUINGILIANO WA MASAFA



  JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
ISO 9001: 2008 CERTIFIED
TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU MUINGILIANO WA MASAFA YA EATV NA ITV KUPITIA KING’AMUZI CHA KAMPUNI YA STAR MEDIA KATIKA KITUO CHA KUSAMBAZA MATANGAZO MAKONGO JUU

  1. UTANGULIZI
  1. Masafa ni rasilimali muhimu katika shughuli za Mawasiliano (simu, wavuti, redio, na utangazaji). Masafa ya Mawasiliano (Spectrum) hugawanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) (ikitambuliwa hapa kama Mamlaka) kwa kutoa leseni kwa watoa huduma za mawasiliano nchini kwa mujibu wa sheria na masharti ya leseni. Moja ya kazi za Mamlaka ni pamoja na kupokea na kusuluhisha matatizo ya muingiliano wa masafa kati ya watoa huduma mbalimbali wa mawasiliano kwa kutumia ujuzi na wataalamu na teknolojia ya mitambo maalumu na mahususi ya kisayansi kufanya kazi hiyo. 
  2. Kazi hizi zimeainishwa katika Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano ya 2003 (TCRA Act of 2003) na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Electronic and Postal Communications Act (EPOCA) ya mwaka 2010.
  3.  
  4. Mnamo tarehe 29 Januari 2015, Mamlaka ilipokea malalamiko kuhusu ubora wa matangazo ya vituo vya ITV na EATV yanayorushwa na Kampuni ya Star Media (T) Limited ambaye ni msambaza matangazo ya dijitali. ITV na EATV wana leseni ya Maudhui (Content Service Lisence) na Star Media wana leseni ya Miundombinu ya Utangazaji (Network Facility License as a signal distributor) kutoka TCRA. Leseni zote za Mamlaka zina masharti ya kuzingatia.
  5. Huduma za Mawasiliano hutumia bendi ya masafa tofauti (Spectrum bands). Huduma za mawasiliano ya setilaiti (satellite) hutumia bendi 3.4 mpaka 4.2 GHz, inayofahamika kama C-Band. Ifahamike kuwa masafa ya setilaiti ya kupokea matangazo (satellite downlink frequency) ya 3.644 GHz yanatumika kupokea matangazo kutoka satelaiti ya Intelsat 906 (TP 10) kwa matangazo ya vituo vya utangazaji nchini kupitia mfumo wa dijitali ambao mitambo yake iko katika kilima cha Makongo Juu area. Hata hivyo, sehemu nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, hutumia teknolojia ya WiMAX katika bendi 3.5 GHz. Masafa haya yanafahamika duniani kote kwa uwezo wake wa kutumika kiteknolojia kati ya mfumo wa “Fixed Satellite Services (FSS)” na IMT kama vile mwendo kazi wa intaneti bila waya (Broadband Wireless Access (BWA) transmission) ikiwemopia  teknolojia ya WiMAX.
4.    Kufuatia malalamiko yaliyopokelewa na Mamlaka, TCRA iliteua timu ya wataalamu Wahandisi wa Masafa kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo la muingiliano wa masafa yaliyosababisha ITV na EATV kutokuonekana vizuri katika king’amuzi cha Star Media, kwa kutumia utaratibu na jinsi sheria zinavyoelekeza. Timu hiyo ya wataalamu wa masafa iliwasiliana na Star Media na kutembelea eneo la Makongo Juu kwenye mitambo yao ili kubaini aina ya muingiliano, muda wa muingiliano na maeneo husika. Timu hiyo ilifanya uchunguzi kwa kutumia vifaa maalumu kwenye eneo lenye mitambo ya kurusha matangazo ili kubaini muingiliano wa masafa kupitia watoa huduma wa intarneti za mwendo kasi kupitia teknolojia ya WiMAX katika bendi 3.4 – 3.6 GHz. Aidha timu ilifanya tathmini ya vipimo vya matumizi ya masafa na watoa huduma katika bendi nzima ya C- ya kupokelea matangazo (downlink frequency) kutoka 3.4 GHz hadi 4.2 GHz.

B.   MATOKEO YA UCHUNGUZI NA YALIYOJITOKEZA

5.    Baada ya uchunguzi huo wa kitaalamu kwa kutumia vifaa maalumu vya teknolojia ya sayansi ya masafa, timu ya wataalamu walibaini kuwa muingiliano wa masafa ulikuwa unatokea kati ya saa 12 jioni hadi saa 6 usiku. Uchunguzi katika eneo la urushaji wa matangazo na mitambo ya Star Media ulibaini kuwa muingiliano ulikuwa katika mfumo wake wa kupokea matangazo (satellite receiver station) iliyoko kwenye eneo (S 06 45’ 736 E 39 12’ 632). Mfumo wa kupokea (Low Noise Block down converter - LNB) kutoka bendi 3.4 GHz to 4.2 GHz. Matokeo ya uchunguzi wa masafa ya bendi 3.644 GHz hayakuonesha aina yeyote ya muingiliano. Aidha masafa ya 3.4 GHz hadi 3.6 GHz yalionesha matumizi mbalimbali kutoka masafa ya bendi 3.5 GHz ambayo yanatumika na watoa huduma wanaotumia teknolojia ya WiMAX.

6.    Kutokana na matokeo ya uchunguzi kama ilivyoelezwa katika no 5, ilibainika wazi kuwa hakukuwa na muingiliano katika bendi hiyo (In-band interference) kutoka katika mfumo wa matumizi ya inteneti ya mwendo kasi kwani masafa yote katika mifumo yote ya utoaji huduma haikuonesha muingiliano. Vile vile ilithibitika wazi kuwa hakukuwa na muingiliano katika mfumo huo (out-of-band emissions) Mfumo wa huduma wa mwendo kasi wa inteneti unaotumia masafa ya bendi 3.5 GHz huweza kusababisha muingiliano kwa mtoa huduma anayetumia bendi 3.6 – 4.2 GHz (FSS stations).

7.    Matokeo ya vipimo vilionesha kuwa eneo la Makongo Juu hupokea mawimbi ya Mawasiliano kutoka kwa watoa huduma wote wanaotumia masafa ya 3.5 GHz kutoka meneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na eneo la Makongo kuwa juu. Hali hii inaweza kusababisha mawimbi ya mwendo kasi wa intaneti katika masafa 3.5 GHz kuibebesha mzigo mkubwa mtambo wa kupokea matangazo ya utangazaji (FSS stations) anayetumia bendi 3.4 – 4.2 GHz kama hakuna wigo wa kuzuia muingiliano kiteknolojia (band pass filter) au mfumo bendi mwembamba (narrow band LNBs).

C.   KUTATULIWA KWA MUINGILIANO WA MASAFA

8.    Kutokana na vielelezo vya matokeo ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa masafa kwa kutumia vifaa maalumu, Mamlaka ilitoa maelekezo kwa Star Media ili kutatua tatizo la muingiliano uliokuwepo katika mtambo wake wa urushaji matangazo Makongo Juu. Kwanza, kutumia kifaa kiitwacho IF attenuator/filter katika mitambo yake ya kupokelea mawasiliano ya matangazo ya setilaiti (FSS receiving station); Kutumia LNB converter katika bendi ya masafa 3.7 – 4.2 GHz badala ya kutumia masafa ya (C-band) yote (3.4 – 4.2 GHz); hata hivyo, masafa 3.664 GHz yamehifadhiwa kama wigo unaozuia matumizi kati ya watumiaji wa matangazo ya mitambo iliyosimikwa juu ya ardhi (Terrestrial) - (3.4-3.6 GHz) na yale ya wanaotumia Satelaiti ya kupokelea matangazo (3.7-4.2 GHz). Pili, Mamlaka ingeagiza watoaji wa inteneti ya mwendo kasi katika mitambo yao (BWA) kuwa na nafasi ya kutosha kati ya mitambo ya “FSS” na kufuata utaratibu uliowekwa kulingana na matumizi ya masafa, ikizingatiwa kwamba mawimbi yaliyo mengi katika eneo la Makongo Juu hupokelewa kutoka sehemu mbalimbali kutoka Jiji la Dar es salaam. Tatu, njia mbadala zitumike katika kupokea matangazo ya utangazaji katika kilima cha Makongo Juu kama vile teknolojia ya Mkongo wa Mawasiliano (fiber optic) satelaiti kutumia mfumo wa bendi ya Ku-Satellite band, au “microwave links”.

9.     Baada ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kufanya uchunguzi wa kitaalamu kwa kutumia vifaa maalumu vya sayansi na teknolojia mahususi kwa matatizo ya muingiliano wa masafa, imebainika pasina shaka kuwa hakukuwa na hujuma yeyote kutoka kwa Kampuni ya Star Media au kufanya kwa makusudi kwa nia ya  kuharibu muonekana wa vituo husika vya ITV na EATV katika ving’amuzi vyake. Tatizo lilikuwa ni la kisayansi na kiteknolojia ambalo hutokea mara nyingi katika huduma za Mawasiliano kote duniani, na tatizo hilo limemalizika kwa kutumia njia za kisayansi na kiteknolojia kwa watoa huduma wote kwa kushirikiana na Mamlaka..

10. Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) inapenda kutumia fursa hii kuwakumbusha watoa huduma wote wenye leseni za Mamlaka kuwa inapotokea matatizo au malalamiko, basi wafuate taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na masharti ya leseni pamoja na kanuni zake ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa TCRA na kutoa ushirikiano katika kutatua tatizo husika kupitia sayansi na teknolojia ambayo hutumika katika kutoa huduma za mawasiliano.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana nasi kupitia dg@tcra.go.tz

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
 5th February 2015
 

No comments:

Post a Comment

Pages