Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Baraka Kizuguto kuwa Ofisa Habari
kuanzia Februari 1 mwaka huu.
Kabla ya
uteuzi huo, Kizuguto alikuwa Ofisa Habari wa klabu ya Young Africans, nafasi
aliyoitumikia kwa miaka miwili.
Kizuguto
ana Stashahada ya Juu ya Habari na Mawasiliano kutoka Chuo cha LEARN IT cha Dar
es Salaam. Pia ana ujuzi wa kusanifu tovuti, ufundi wa kompyuta na uchambuzi wa
mifumo ya kompyuta.
Mei mwaka
jana, Kizuguto aliteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
kuhudhuria mafunzo ya usajili na uhamisho wa kimataifa wa wachezaji kwa njia ya
mtandao (TMS) yaliyofanyika Johannesburg, Afrika Kusini.
TFF
inamtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya.
KAMATI YA NIDHAMU YAADHIBU TISA
Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa adhabu kwa watu
tisa wakiwemo viongozi, wachezaji na kocha mmoja kwa kupatikana na hatia ya
makosa ya kinidhamu.
Katika
kikao chake kilichofanyika juzi (Februari 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam,
Kamati hiyo imewafungia mwaka mmoja viongozi wawili wa Chama cha Mpira wa Miguu
wa Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza
Queens kugomea uamuzi halali.
Sophia
Tigalyoma (Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa Bajanguo walitiwa hatiani kwa
kuwashawishi wachezaji kugomea uamuzi wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake
ya TFF kutupa rufani yao dhidi ya Kigoma.
Kocha wa
Polisi Tabora, Eliakim Christopher amefungiwa mechi kumi na kupigwa faini ya
sh. 300,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 39(2) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada
ya kutiwa hatiani kwa kumtukana refa wakati wa mechi kati ya timu yake na
Panone FC iliyochezwa mjini Moshi.
Wachezaji
wa JKT Oljoro FC, Dihe Makonga, Swaleh Idd Hussein, Ramadhan Mnyambegu na
nahodha Shaibu Nayopa wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 300,000 kila mmoja
kwa kuzingatia kanuni ya 36(10) ya FDL kutokana na kufanya vurugu kwenye mechi
kati yao na Burkina Faso iliyochezwa mjini Morogoro.
Mtunza Vifaa
(Kit Man) wa JKT Oljoro FC, Eliud Mjarifu amefungiwa miezi sita na kupigwa
faini ya sh. 200,000 kwa kumpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi
kati ya timu hizo iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Pia Mjarifu
amepewa onyo kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani hata mwenendo
wake wakati wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu mbele ya Kamati.
Naye
Mtunza Vifaa wa Rhino Rangers FC, Albert Mbuji amefungiwa miezi sita na faini
ya sh. 200,000 kwa kupatikana na hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa
kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa
kanuni ya 40(2) ya FDL.
Kamati
hiyo imeondoa malalamiko dhidi ya Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau
Bwire kwa vile refa Israel Mujuni Nkongo ambaye ni mlalamikaji hakufika kwenye
shauri hilo.
Nkongo
alimlalamikia Bwire akidai alitoa maneno yenye kuweza kuchochea chuki dhidi
yake kwa waamuzi, kwani kupitia redio 100.5 Times FM, Bwire alidai refa huyo
ndiye aliyeshinikiza kuondolewa kwa refa Mohamed Theofil kwenye ratiba ya Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL).
Pia Kamati
hiyo imemkuta bila hatia Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Singida (SIREFA), Gabriel Gunda ambaye TFF ilimlalamikia kuwa akiwa mtendaji
mkuu wa chama hicho alishindwa kuhakikisha timu ya Singida inaingia uwanjani
kucheza na Dodoma kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake.
Kamati
ilikubaliana na utetezi wa Gunda kuwa, jukumu la timu hiyo lilikuwa mikononi
mwa viongozi wa TWFA Singida, na tayari SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu
ilishatoa adhabu kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kitendo hicho.
Nayo
malalamiko ya Polisi Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC
irudiwe kwenye uwanja huru (neutral ground) kwa madai ya kuchezeshwa zaidi ya
muda unaotakiwa, na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza yamekataliwa.
Pia Kamati
ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi
ya Toto Africans kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni
yake yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya
kinidhamu.
Wakati
huo huo, Kamati ya Nidhamu inaendelea na kikao chake leo (Februari 5 mwaka huu)
kusikiliza malalamiko mengine ya kinidhamu yaliyofikishwa mbele yake.
TFF YAONYA KUHUSU UENDESHAJI
MPIRA WA MIGUU
Kutokana
na matatizo mbalimbali ya kiutendaji yaliyojitokeza kwenye uendeshaji,
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa hadhari kuwa shughuli zote
za mpira wa miguu zinazohusu mkoa wowote wa Tanzania Bara zitasimamiwa na Chama
cha Mpira wa Miguu cha Mkoa husika, yakiwemo mashindano ya Kombe la Taifa la
Wanawake.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment