April 07, 2015

Askofu Mshana; Akemea Kanisa si mahali pa Biashara

NA BRYCESON MATHIAS, DODOMA

MSAIDIZI wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Dodoma, Samwel Mshana, amekemea vikali na kuwaonya waandaaji wa Tamasha la Tangaza Amani, Imba na Badilisha Kipato kuwa Ajira, kwamba kanisani si mahali pa biashara bali ni nyumba ya ibada.

Askofu Mshana alisema hayo Jumatatu, Aprili 6, kwenye Pasaka ya Pili, ambapo kwenye Tamasha la Uimbaji wa Kwaya mbalimbali lililoandaliwa na RASI FM Radio yenye masafa ya 103:7 FM, kwenye ratiba yao waliweka tukio la kukata keki ya biashara (pichani) yenye umbo la kanisa.

Keki yenye umbo la Kanisa iliyokusudiwa iuzwe kanisani KKKT, Usharika wa Kanisa Kuu Dodoma, ambapo Msaidizi wa Askofu, ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Samwel Mshana, alikataa kanisa lake kufanywa mahali pa biashara.

Akifungua tamasha hilo kwenye Kanisa Kuu la KKKT Dodoma, Askofu Mshana, ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, ili kulinda maadili ya kanisa, aliwajia juu waandaaji hao akisema ana mambo matatu ambayo hayakumfurahisha wanayotakiwa kuyakomesha mara moja.

“Waandaaji mmeshindwa kuzingatia muda, mlisema tamasha litaanza saa sita mchana na mimi askofu nitafungua tamasha hilo saa tisa (15:10-15:40), lakini hadi saa nane hii ndiyo kwanza mnaanza, ikiwa hivyo, siku nyingine msiniite, sitakuja!
“Kwenye ratiba yenu kipengele cha tisa, mmeonyesha kuna kukata keki ya biashara, napenda niwaonye kanisani si mahali pa biashara, hivyo sitaki kuona kwenye Kanisa lolote la KKKT Dodoma ninaloliongoza kunafanywa biashara, kama kuna biashara hiyo ikafanyiwe nje ya kanisa,” alikemea Mshana.

Alionya kuwa kanisa ni mahali pa kusifu na kuabudu; ni nyumba ya ibada, ambapo watu wanaomba, wanaimba na kuponywa magonjwa, huzuni na taabu zao, ili wapate furaha na  kuhuishwa uhai wa kiroho na miili yao! Lakini katu si mahali pa kufanya biashara. 

Alisema tunasoma katika Luka 19:45; “(Yesu); Akaingia hekaluni akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, imeandikwa, nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Msifanye hivyo hapa!
Baada ya Kiongozi wa uandaaji wa tamasha hilo kukiri kuwepo makosa ya uchapaji na kwamba tukio hilo halitafanyika, Askofu Mshana alifungua uimbaji huo akiwataka waimbaji wawe kama mwanamke, Mariamu Magadalene, ambaye alijua umuhimu wa Kanisa na Yesu, aliyemponya, kiasi cha kufika kaburini alipozikwa ili ampake manukato. 

Waumini na wadau wa habari, walishangazwa na waandaji hao ambao ni wanahabari, kushindwa kujali muda, jambo ambalo ni kubwa na muhimu katika fani ya kazi yao ili kuweza kuwahi matukio ya uandishi wa habari za radio, TV na magazeti.
Keki yenye umbo la Kanisa la iliyokusudiwa iuzwe kanisani KKKT Usharika wa Kanisa Kuu Dodoma, ambapo Msaidi wa Askofu ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Samwel Mshana alikata Kanisa lake kufanywa mahali pa Biashara.

No comments:

Post a Comment

Pages