April 08, 2015

Chadema kumng’oa mwenyekiti wa CCM

NA BRYCESON MATHIAS, MOROGORO

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tawi la Mbigili wilayani Kilosa, kimesema kitamng’oa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hemed Ibrahim Salim, kama ataendelea kutoitisha vikao kwa kisingizio cha kuogopa kukataliwa kwa kukosa taarifa ya makabidhiano.

Akizungumza mtandao huu, Mwenyekiti wa Chadema wa tawi hilo, Maftaha Hamis, alimtuhuhu mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho kwamba alichapisha vitabu vya risiti za michango kwa ajili ya ufuatiliaji wa mgogoro wa wakulima na wafugaji, ikidaiwa fedha hizo zilizokusanywa zimetafunwa.

Awali ilifahamika kwamba, Mwenyekiti Salum anabanwa kuhusu taarifa ya makabidhiano ya serikali ya Kijiji hicho kwa sababu, kabla ya kuchaguliwa Desemba 14, mwaka jana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa mpito, baada ya aliyekuwa mwenyekiti kujiuzulu.

Hamisi alisema: “Kuna risiti feki alizochapisha na kugonga mhuri wa halmashauri kisiri, ambapo wakulima waliopo kijijini cha mbigili, walichangishwa sh. 2,000 na wakulima wa Mbigili wanaoishi Morogoro mjini walichangia sh. 5,000, lakini kwa masikitiko, fedha hizo zilitafunwa.”

Mbali ya fedha zenye risiti feki kutafunwa, Mwenyekiti Hamis wa Chadema alidai sababu nyingine za kumng’oa Mwenyekiti wa CCM, Salim, ni pamoja na sintofahamu ya ziliko fedha za ruzuku ya kijiji sh. milioni 15 na mifuko ya saruji 50 za Mfuko wa Maendeleo wa Rais (TASAF), ambazo hazijulikani ziliko.

Aidha Hamis aliongeza kutoa madai kwamba, bado kuna sintofahamu kuhusu Shule ya Sekondari ya Mazoezi ya Mbigili, ambayo imekuwa haifahamiki kama imesajiliwa au la, kwa sababu tayari imetumia fedha nyingi kuikarabati na wananchi wamechangia nguvu zao kwa kiwango kikubwa.

Awali Mwenyekiti Salim alipohojiwa dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake, alikanusha vikali na kudai kuhusu mifuko 50 ya saruji, anatakiwa ahojiwe aliyekuwa mwenyekiti kabla yake, ili kujua waliitumiaje na aliyekuwa mkandarasi wa Sekondari ya Magore, na kuhusu sh. mil. 15, alisema zilipopelekwa kijijini hapo zilipokewa zikiwa na maagizo ya uongozi wa Wilaya ya Kilosa ya nini zifanyike.

No comments:

Post a Comment

Pages