April 23, 2015

Mchungaji TAG: Nimepata wito kuitumikia Chadema

Na Bryceson Mathias, Morogoro Vijijini

MCHUNGAJI wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Morogoro, James Samson Mabula (Power Mabula), amesema baada ya kuitwa na Mungu kwenye uchungaji, ndani mwake Mungu amempa wito wa kukitumikia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). 

Akizungumza katika mikutano ya kujinadi baada ya kutia nia ya kutaka kugombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi ya (Chadema), Mabula ambaye aliwahi kuteuliwa na Askofu Mkuu wa TAG, Barnabas Mtokambali, kuwa Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Bethel Revival alisema:

“Nilipata wito wa kukitumikia Chadema katika siasa na kujiunga nacho mapema kabisa, kwa sababu ndicho chama pekee nilichoona kina nia ya dhati ya kuwakomboa Watanzania, na sasa ukiwemo Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

“Nikiwa Chadema, baada ya kuona baadhi ya wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambao hawamo katika Umoja wa UKAWA si waadilifu na hawana mzigo wa kuwatumikia wananchi, nimepata wito wa kutia nia ya kugombea ubunge Morogoro, Chadema inifikirie,” alisema Mabula.

Mabula alisema iwapo Chadema itampa ridhaa kusimama katika kinyang’anyiro hicho na akashinda ubunge, moja ya mambo Matano makuu atakayofanya akishirikiana na chama chake ni kuhakikisha anarudisha kwa wananchi  viwanda 11 vilivyouawa na serikali ya CCM.

Aidha, amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuhakikisha huduma ya maji inavifikia vijiji vyote 29 vya Manispaa ya Morogoro, huku akihakikisha anaungana na wabunge wenzake watakaoshinda kuilazimisha serikali kulinda rasilimali za wananchi zinazoporwa kila kukicha.

Wanachama 11 wa Chadema wametangaza nia ya kutaka kuwania Jimbo la Morogoro Mjini, ambalo kwa sasa linaongozwa na  Abdul-Aziz Mohamed Abood (CCM), ambapo miongoni mwao yumo mwanasheria Bathromeo Tarimo, tayari wanapiga jalamba  katika kata 29 kujinadi kwa wanachama ili wakubaliwe  na chama.

No comments:

Post a Comment

Pages