April 01, 2015

Waumini waunga mkono maaskofu kumjibu Rais Kikwete

Na Bryceson Mathias, Dodoma

 

WAUMINI wengi wa madhehebu ya Kikristo waliohojiwa kwa nyakati tofauti mkoani Dodoma wameunga mkono hatua ya maaskofu kumjibu Rais Jakaya Kikwete kutokana na kusema tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa lilikuwa la hasira.

Waumini hao wamewaunga mkono maaskofu kufuatia viongozi hao kujitokeza tena na kusisitiza kwamba msimamo wao utabaki kama ulivyo, ikiwa ni siku tano baada ya Rais   Kikwete akiwa ameongea na watu wengine si wao.

Katika tamko la pamoja walilolitoa mwanzoni mwa wiki hii mkoani Dodoma  baada ya kukutana, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza kulitumbukiza taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo s
serikali ndiyo ilaumiwe.

Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali Machi 12, mwaka huu yaani Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.

Tamko hilo lenye maneno 921, limeendelea kuwataka waumini wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya ‘hapana,’.

Msimamo huo wa maaskofu, tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya kura wanayostahili kupiga.

Kwa upande wa waumini waliohojiwa wamedai, hata wao hawamuelewi pengo anaposema, viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya kura wanayostahili kupiga, hivyo wanahoji, mbona viongozi wa serikali akiwemo rais na mawaziri, wanawaamulia waumini wa kiroho wapige kura ya ‘Ndiyo?’


Wengine wamekwenda mbali wakisema, historia ya kanisa kamwe haisemi hata siku moja kama serikali iliwahi kuliongoza kanisa, isipokuwa kanisa ndilo lililokuwa linaiongoza serikali, hivyo mkanganyiko huo ndio usipofikiwa maridhiano lazima uigharimu serikali.“Ni vigumu watawala waingie kusema vitu kanisani, misikitini, halafu wenye makanisa na misikiti wasiseme kitu kwenye serikali, wakae kimya kama vinyago, hilo halikuwa jambo la busara na hekima mbele za Mungu na watu,”  alisema Benjamin Kambangwa wa Kanisa Katoliki.

Naye Josephina James wa Kanisa la Anglikana alisema, viongozi wakuu wa serikali – Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete wasifurahie wakidhani ujumbe wao walioongea na viongozi wa Kikristo wasiostahili umewafikia viongozi wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu waliokutana nao si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au kukubaliana juu ya jambo hilo la kitaifa.

Joachim Jackson wa Evangelistic Assemblies of God alisema rais kuzungumza na wazee wa Dar es Salaam na mkuu wa mkoa na kutafsiri kuwa viongozi wa dini wana hasira wakati hawaongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi, ni kutowatendea haki, maana wao wanaongozwa na maombi na sala, hivyo wanatakiwa waombwe radhi.

Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘Hapana’ Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.

“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete.
Kikwete aliongeza: “Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao... hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa serikali kupeleka bungeni muswada wa Mahakama ya Kadhi.”

Maaskofu hao walikuwa Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964 unaotambua Mahakama ya Kadhi.

No comments:

Post a Comment

Pages